Generic placeholder image

Agosti 15
KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Nani huyu aliyepaa juu
Baada ya Mfalme wa mbingu?
Malaika waimba zake sifa
Huku waruka na kumzunguka!

Nani huyu alopambwa kwa nuru,
Jua mwilini mwake kalivaa,
Migu'ni malkia wa usiku
Tufe libadilikalo kaweka?

Huyu ndo alomchukua mimba
Mfalme wa Mbingu kwa miezi;
Kwa hiyo huyu hawezi kubaki
Katika kaburi la duniani.

Alikuwa mbingu, moto kashika,
Asili ya mwanga wa ulimwengu,
Sasa miali ya moto yataka
Kwenda mbinguni na kuunganika.

Yeye vizuri aliyeangaza
Siku yetu ilipoanza kuwa,
Tazama mwanga wake wafifia
Kwa vile sasa kaketi na Jua.

ANT. I: Kristo alipopaa mbinguni, alitayarisha huko makao ya kudumu kwa ajili ya Mama yake, Bikira safi kuliko wote, aleluya.

Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!

Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.

Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!

Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.

Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;

lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.

Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Kristo alipopaa mbinguni, alitayarisha huko makao ya kudumu kwa ajili ya Mama yake, Bikira safi kuliko wote, aleluya.

ANT. II: Watu wote walifungiwa milango ya paradisi kwa sababu ya Eva, lakini milango hiyo imefunguliwa tena kwa njia ya Bikira Maria, aleluya.

Zab.147:12-20 Ni vizuri kumsifu Mungu
Ee Yerusalemu, umsifu Mungu!*
Umsifu Mungu wako, ee Sion!

Maana ameiimarisha milango yako,*
amewabariki watu waliomo kwako.

Ameweka amani mipakani mwako;*
anakushibisha kwa ngano safi kabisa.

Yeye hupeleka amri yake duniani,*
na neno lake hutekelezwa upesi.

Hutandaza theluji kama pamba,*
hutawanya umande kama majivu.

Huleta mvua ya mawe/
vipande vikubwa vikubwa kama mkate*
na kwa ubaridi wake maji huganda.

Kisha hutoa amri, na maji hayo huyeyuka;*
huvumisha upepo wake, nayo hutiririka.

Humjulisha Yakobo ujumbe wake,*
na Israeli amri na maagizo yake.

Lakini watu wengine hakuwafanyia hayo;*
watu wengine hawayajui maagizo yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Watu wote walifungiwa milango ya paradisi kwa sababu ya Eva, lakini milango hiyo imefunguliwa tena kwa njia ya Bikira Maria, aleluya.

ANT. III: Bikira Maria amepalizwa juu mbinguni; njooni, sote tumtukuze Kristo mfalme, ambaye utawala wake hauna mwisho.

WIMBO: Efe.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Bikira Maria amepalizwa juu mbinguni; njooni, sote tumtukuze Kristo mfalme, ambaye utawala wake hauna mwisho.

SOMO: Rom.8:30
Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita aliwafanya pia wawe na uhusiano mwema naye; na hao aliowafanya wawe na uhusiano mwema naye aliwashirikisha pia utukufu wake.

KIITIKIZANO
K. Maria amepalizwa mbinguni; malaika wanafurahi. (W. Warudie)
K. Wanaimba kwa furaha, na kumsifu Bwana.
W. Malaika wanafurahi.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Maria...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tazama, watu wote wataniita mwenye heri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tazama, watu wote wataniita mwenye heri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, aleluya.

MAOMBI
Tumtukuze Mungu Baba, aliyemchagua Maria awe mama ya Mwanae, na aliyetaka vizazi vyote vimwite ni mwenye heri. Kwa imani na matumaini, tuombe:
W. Maria Mtakatifu, utuombee.

Baba, ulifanya mambo makuu kwa ajili ya Bikira Maria, na ukamfikisha, mwili na roho, kwenye utukufu wa mbinguni;
- uijaze mioyo ya watoto wako matumaini ya kupata utukufu wa Kristo. (W.)

Kwa maombezi ya Maria, mama yetu, uwaponye wagonjwa, uwatulize wenye huzuni, uwasamehe wenye dhambi;
- uwajalie watu wote amani na wokovu. (W.)

Ulimjalia Maria neema tele;
- uwashushie watu wote baraka zako kwa wingi. (W.)

Uliunganishe Kanisa, liwe moyo mmoja na roho moja, kwa nguvu ya upendo;
- na uwawezeshe waamini wako kujiunga na Maria, mama ya Yesu, katika kusali daima. (W.)

Baba, umemtukuza Bikira Maria, na kumfanya awe malkia wa mbingu;
- uwajalie marehemu kuingia katika ufalme wako, na kufurahi pamoja na watakatifu wako milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Baba yetu, ulimvika Bikira Maria taji ya utukufu usio na kifani siku alipopalizwa mbinguni. Uliutazama unyonge wake, na ukamfanya awe mama ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao wa Pekee. Kwa sala zake, utujalie tuweze kuokolewa kwa fumbo la ukombozi uliotupatia, na kushiriki pamoja naye utukufu wa uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.