Generic placeholder image

Agosti 15
KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Nani huyu aliyepaa juu
Baada ya Mfalme wa mbingu?
Malaika waimba zake sifa
Huku waruka na kumzunguka!

Nani huyu alopambwa kwa nuru,
Jua mwilini mwake kalivaa,
Migu'ni malkia wa usiku
Tufe libadilikalo kaweka?

Huyu ndo alomchukua mimba
Mfalme wa Mbingu kwa miezi;
Kwa hiyo huyu hawezi kubaki
Katika kaburi la duniani.

Alikuwa mbingu, moto kashika,
Asili ya mwanga wa ulimwengu,
Sasa miali ya moto yataka
Kwenda mbinguni na kuunganika.

Yeye vizuri aliyeangaza
Siku yetu ilipoanza kuwa,
Tazama mwanga wake wafifia
Kwa vile sasa kaketi na Jua.

ANT. I: Maria amepalizwa mbinguni, malaika wanafurahi. Wanaimba kwa furaha, na kumsifu Bwana.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Maria amepalizwa mbinguni, malaika wanafurahi. Wanaimba kwa furaha, na kumsifu Bwana.

ANT. II: Bikira Maria amepalizwa na kuingizwa katika makao ya mbinguni, ambako Mfalme wa wafaIme amekalia nyota.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Bikira Maria amepalizwa na kuingizwa katika makao ya mbinguni, ambako Mfalme wa wafaIme amekalia nyota.

ANT. III: Wewe, Ee binti, umebarikiwa na Bwana; kwa njia yako tumeshiriki tunda la uzima.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Wewe, Ee binti, umebarikiwa na Bwana; kwa njia yako tumeshiriki tunda la uzima.

SOMO: 1Kor.15:22-23
Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo. Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza; halafu wale walio wake Kristo, wakati Kristo atakapokuja.

KIITIKIZANO
K. Bikira Maria amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika. (W. Warudie)
K. Atukuzwe Bwana, aliyempaliza yeye juu.
W. Juu zaidi kuliko makundi ya malaika.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bikira...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Leo Bikira Maria alipalizwa mbinguni; furahini na shangilieni, maana atatawala milele na Kristo.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Leo Bikira Maria alipalizwa mbinguni; furahini na shangilieni, maana atatawala milele na Kristo.

MAOMBI
Tumtukuze Mungu Baba, aliyemchagua Maria awe mama ya Mwanae, na aliyetaka vizazi vyote vimwite ni mwenye heri. Kwa imani na matumaini, tuombe:
W. Maria Mtakatifu, utuombee.

Baba, ulifanya mambo makuu kwa ajili ya Bikira Maria, na ukamfikisha, mwili na roho, kwenye utukufu wa mbinguni;
- uijaze mioyo ya watoto wako matumaini ya kupata utukufu wa Kristo. (W.)

Kwa maombezi ya Maria, mama yetu, uwaponye wagonjwa, uwatulize wenye huzuni, uwasamehe wenye dhambi;
- uwajalie watu wote amani na wokovu. (W.)

Ulimjalia Maria neema tele;
- uwashushie watu wote baraka zako kwa wingi. (W.)

Uliunganishe Kanisa lako liwe moyo mmoja na roho moja, kwa nguvu ya upendo;
- na uwawezeshe waamini wako kujiunga na Maria, mama ya Yesu, katika kusali daima. (W.)

Baba, umemtukuza Bikira Maria, na kumfanya awe malkia wa mbingu;
- uwajalie marehemu kuingia katika ufalme wako, na kufurahi pamoja na watakatifu wako milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, umempaliza, mwili na roho, Bikira Maria asiye na doa, mama ya Mwanao, na kumwingiza katika utukufu wa mbinguni. Uielekeze mioyo yetu mbinguni, ili, pamoja naye, tuweze kushiriki utukufu wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.