Generic placeholder image

Agosti 15
KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
SALA ZA MCHANA

chagua SALA YA ADHUHURI
chagua SALA KABLA YA ADHUHURI
Kwa SALA BAADA YA ADHUHURI: endelea hapo chini

BAADA YA ADHUHURI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina (Aleluya)

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;.
Na yote yanafanyika.
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu.
Milele inayodumu.

ANT.: Mama Mtakatifu wa Mungu, amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika, na ameingia katika ufalme wa mbinguni.

Zab.126 Kuomba nguvu mpya
Mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu (2Kor.1:7)

Mungu alipoturudisha tena Sion,*
tulikuwa kama wanaoota ndoto!

Hapo tuliangua kicheko;*
tulishangilia kwa furaha.

Nao watu wa mataifa mengine walisema,*
"Mungu amewatendea mambo makubwa!"

Kweli Mungu alitutendea maajabu,*
tulifurahi kweli kweli!

Ee Mungu, urekebishe tena hali yetu,/
kama mvua inavyotiririsha maji*
katika mabonde makavu.

Wanaopanda kwa machozi*
watavuna kwa shangwe.

Wanaokwenda kupanda mbegu huku wakilia,*
watarudi kwa furaha huku wakichukua mavuno.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Ninyi ni jengo lake Mungu (1Kor.3:9)

Mungu asipoijenga nyumba,*.
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.128 Tuzo kwa jamaa imchayo Mungu
'Bwana akubariki kutoka Sion', yaani kutoka Kanisa lake (Arnobius)

Heri wote wamchao Mungu,*
Wanaoishi kufuatana na amri zake.

Kazi zako zitakupatia mahitaji yako,*
utaona furaha na kufanikiwa.

Mke wako atakuwa kama mzabibu*
wenye matunda mengi nyumbani mwako;

watoto wako watakuwa kama machipukizi*
ya mizeituni kuizunguka meza yako.

Naam, ndivyo atakavyobarikiwa*
mtu amchaye Mungu.

Mungu akubariki toka Sion!*
Uione fanaka ya Yerusalemu,

siku zote za maisha yako.*
Uishi na hata uwaone wajukuu wako!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant.: Mama Mtakatifu wa Mungu, amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika, na ameingia katika ufalme wa mbinguni.

SOMO: 2Kor.5:1
Tunajua kwamba hema hii ambayo ndani yake tunaishi sasa hapa duniani, yaani mwili wetu, itakapong'olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono.

K. Bikira Maria amepalizwa, na kuingizwa katika makao ya mbinguni.
W. Huko Mfalme wa wafalme amekalia nyota.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi wa milele, umempaliza, mwili na roho, Bikira Maria asiye na doa, mama ya Mwanao, na kumwingiza katika utukufu wa mbinguni. Uielekeze mioyo yetu mbinguni, ili, pamoja naye, tuweze kushiriki utukufu wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.