Generic placeholder image

Agosti 21
MTAKATIFU PIO X Papa
JUMATANO JUMA LA 20 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

E Mungu hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Baba, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nimewatuma hao ulimwenguni (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Mtu anayewapokea ninyi, hunipokea mimi: yeyote anayenipokea mimi, humpokea Yeye aliyenituma (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Sisi twafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni bustani ya Mungu, ni jengo la Mungu (aleluya).

Zab.119:145-152 XIX Kuomba usalama
Nakulilia kwa moyo wangu wote;/
unisikilize, Ee Mungu,*
nami nitazishika kanuni zako.

Nakulilia, unisalimishe;*
nipate kuyashika mafundisho yako.

Asubuhi na mapema naamka niombe msaada;*
nitaitumainia kabisa ahadi yako.

Nakaa macho usiku kucha,*
ili niyatafakari maagizo yako.

Kwa upendo wako mkuu, Ee Mungu, unisikilize;*
uoneshe huruma yako, ukanisalimishe.

Wadhalimu wangu wakatili wanakaribia,*
watu ambao hawaishiki kamwe sheria yako.

Lakini wewe u karibu nami, Ee Mungu,*
na maagizo yako yote ni ya kuaminika.

Tangu zamani nimejifunza maagizo yako;*
wewe umeyaweka yadumu hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.94 Mungu hakimu wa wote
Bwana atawaadhibu wenye dhambi: maana Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali alituita tuishi katika utakatifu (1Tes.4:6-7)

I
Ee Mungu, Mungu mwenye kutoa adhabu,*
ewe Mungu mwenye kutoa adhabu, ujitokeze!

Usimame, ee hakimu wa watu wote;*
uwaadhibu wenye kiburi wanavyostahili!

Waovu wataona fahari hata lini?*
Watajisifia mpaka lini, Ee Mungu?

Hata lini waovu watajigamba kwa maneno?*
Watajivuna na kujitapa mpaka lini?

Wanawaangamiza watu wako, Ee Mungu,*
wanawakandamiza hao walio mali yako.

Wanawaua wajane na wageni;*
wanawachinja yatima!

Ati wanasema: “Mungu haoni;*
Mungu wa Yakobo hajui!”

Enyi wajinga wa mwisho, fikirini kidogo!*
Enyi wapumbavu, mtapata lini maarifa?

Aliyefanya sikio, je, yeye hawezi kusikia?*
Aliyeumba jicho, je, yeye hawezi kuona?

Mwenye kuyatawala mataifa, hawezi kuadhibu?/
Mkufunzi wa wanadamu, je, hana maarifa?*
Mungu ajua mawazo ya watu kuwa hayafai.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Ee Mungu, heri mtu unayempa nidhamu,*
mtu unayemfundisha sheria yako.

Wakati wa taabu utampa kitulizo,*
hali waovu wanachimbiwa shimo.

Hakika Mungu hatawaacha watu wake;*
hatawasahau hao walio mali yake.

Basi, hukumu zitakuwa za haki tena,*
na waadilifu wote watazizingatia.

Nani aliyenisaidia kumpinga mtu mwovu?*
Nani aliyekuwa upande wangu dhidi ya wabaya?

Mungu asingalinisaidia,*
ningalikwisha enda kwenye nchi ya wafu.

Niliposema: “Naanguka,”*
upendo wako mkuu, Ee Mungu, ulinitegemeza.

Mahangaiko ya moyo wangu yanapozidi,*
wewe wanituliza na kunifurahisha.

Wewe huwezi kuhusiana na watawala dhalimu,*
wanaotunga sheria za kutetea maovu.

Wao wanaafikiana kuwaangamiza waadilifu,*
na kuwahukumu kifo watu wasio na hatia.

Lakini Mungu ni mlinzi wangu thabiti;*
Mungu wangu, ni mwamba wa usalama wangu.

Uovu wao atawarudishia wao wenyewe,/
atawafutilia mbali kwa sababu ya ubaya wao.*
Naam, Mungu, Mungu wetu, atawaangamiza!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Baba, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nimewatuma hao ulimwenguni (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Mtu anayewapokea ninyi, hunipokea mimi: yeyote anayenipokea mimi, humpokea Yeye aliyenituma (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Sisi twafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni bustani ya Mungu, ni jengo la Mungu (aleluya).

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Tim.4:16
Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo, maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.

K. Bwana alimchagua mtumishi wake (aleluya).
W. Alimwita awe mchungaji wa Yakobo, urithi wake (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Tim.1:12
Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo, aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie.

K. Sitaona aibu kutangaza Habari Njema (aleluya).
W. Uwezo wa Mungu ndio unaowaokoa watu (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Tim.3:13
Wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu.

K. Kama Bwana haijengi nyumba hiyo (aleluya).
W. Wale waijengao wafanya kazi bure (aleluya).

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulimjaza hekima Mtakatifu Papa Pio, na ulimpa bidii na uwezo wa kitume ili aitetee imani Katoliki, na avifanye vyote upya katika Kristo. Utujalie tuweze kufuata mfano wake na mafundisho yake, na hivi tulifikie tuzo letu mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.