Generic placeholder image

Agosti 22
MARIA, MALKIA NA MAMA YETU
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bikira, na papo hapo ni Mama,
Binti yake Mwana wako mwenyewe,
U juu kuliko wengine wote
Ila hapana wa chini zaidi;
Wewe ndio utimilifu wote
Ulopangwa kwa amri ya Mungu
Ulimwengu wetu uloanguka
Katika wewe lipokuwa bora!

Akisha tayarishiwa mahali,
Yeye aliyeumba vitu vyote
Kakaa kati ya viumbe vyake,
Kifuani pako ndo akalala;
Hapo akalisha upendo wake
Kwa joto ambalo liliukuza
Mzizi ule ulostawisha
Amani yetu sisi ya milele.

Na si peke yako usikiaye
Sisi tunaposifu lako jina;
Mara nyingi huwa karibu sana
Sauti zetu zinapokatika;
Viumbe vyote kaumbwa vizuri
Kwa umbo na kwa sura yako nzuri,
Huruma, nguvu, upole na wema,
Na neema umejaliwa mama.

Bibi, tushindwapo kuona mbele,
Katika kutarajia ya mbingu,
Endelea bado kutuombea
Sisi kwa huyo Mwanao daima,
Ambaye anastahili sifa,
Nguvu na enzi na wote uweza,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Na pamoja na Baba mtukufu.

ANT. I: Salamu Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe (aleluya).

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Salamu Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe (aleluya).

ANT. II: Mimi ni mtumishi wa Bwana; na iwe kama ulivyosema (aleluya).

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Mimi ni mtumishi wa Bwana; na iwe kama ulivyosema (aleluya).

ANT. III: Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mzao wako amebarikiwa (aleluya).

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mzao wako amebarikiwa (aleluya).

SOMO: Gal.4:4-5
Wakati ule maalum ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria, apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria, ili sisi tufanywe wana wa Mungu.

KIITIKIZANO
K. Salamu Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe. (W. Warudie)
K. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mzao wako amebarikiwa.
W. Bwana yu nawe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Salamu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Umebarikiwa, Ee Bikira Maria, kwa sababu uliamini yote uliyoambiwa na Bwana: utatawala milele pamoja na Kristo.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Umebarikiwa, Ee Bikira Maria, kwa sababu uliamini yote uliyoambiwa na Bwana: utatawala milele pamoja na Kristo.

MAOMBI
Tumtukuze Mungu Baba, aliyemchagua Maria awe mama ya Mwanae, na aliyetaka vizazi vyote vimwite ni mwenye heri. Kwa imani na matumaini, tuombe:
W. Bikira Maria atuombee.

Baba, ulifanya mambo makuu kwa ajili ya Bikira Maria, na ukamfikisha, mwili na roho, kwenye utukufu wa mbinguni;
- uijaze mioyo ya watoto wako matumaini ya kupata utukufu wa Kristo. (W.)

Kwa maombezi ya Maria, mama yetu, uwaponye wagonjwa, uwatulize wenye huzuni, uwasamehe wenye dhambi;
- uwajalie watu wote amani na wokovu. (W.)

Ulimjalia Maria neema tele;
- uwashushie watu wote baraka zako kwa wingi. (W.)

Uliunganishe Kanisa lako liwe moyo mmoja na roho moja, kwa nguvu ya upendo;
- na uwawezeshe waamini wako kujiunga na Maria, mama ya Yesu, katika kusali daima. (W.)

Baba, umemtukuza Bikira Maria, na kumfanya awe malkia wa mbingu;
- uwajalie marehemu kuingia katika ufalme wako, na kufurahi pamoja na watakatifu wako milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi Baba yetu, umetupatia Maria, Mama ya Mwanao, awe Mama yetu na Malkia wetu. Kwa msaada wa sala zake, utuwezeshe kuufikia ufaIme wa mbinguni na utukufu uliowatayarishia watoto wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.