Generic placeholder image

Agosti 28
MTAKATIFU AUGUSTINO Askofu na Mwalimu wa Kanisa
JUMATANO JUMA LA 21 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Baba, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nimewatuma hao ulimwenguni (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Mtu anayewapokea ninyi, hunipokea mimi: yeyote anayenipokea mimi, humpokea Yeye aliyenituma (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Sisi twafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni bustani ya Mungu, ni jengo la Mungu (aleluya).

Zab.119:9-16 II Uaminifu kwa Sheria ya Mungu
Kijana atatunzaje mwenendo wake uwe safi?*
Kwa kuyashika maagizo yako.

Najitahidi kukutii kwa moyo wote;*
unijalie kuzishika amri zako.

Nimeshika agizo lako moyoni mwangu,*
nisije nikakukosea.

Utukuzwe, Ee Mungu!*
Unifundishe kanuni zako.

Nitazirudia kwa sauti*
sheria zako zote ulizotoa.

Nafurahi kufuata amri zako,*
kuliko kuwa na utajiri mwingi.

Nazitafakari amri zako,*
na kuyazingatia maagizo yako.

Nazifurahia kanuni zako;*
sitazisahau amri zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.17 Sala ya mtu mwema
Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye akasikilizwa (Ebr.5:7)

I
Ee Mungu, unisikilize niombapo haki zangu;/
usikilize kilio changu,*
upokee ombi langu la moyo mnyofu.

Utatoa hukumu ya kunifadhili,*
kwani wewe wajua jambo la haki.

Wewe waujua kabisa moyo wangu;/
umenijia usiku, umenichunguza;*
hukuona uovu wowote ndani yangu.

Sisemi maovu, kama wafanyavyo wengine;*
nimeitii amri yako, sikuishika njia ya wadhalimu.

Nimefuata daima njia yako;*
wala sikuiacha kamwe.

Nakuita, Ee Mungu, kwani wanisikiliza;*
unitegee sikio, uyasikilize maneno yangu.

Onyesha upendo wako mkuu,/
uwaokoe kutoka kwa adui zao,*
wale wanaokukimbilia.

Unilinde kama mboni ya jicho lako;/
unifiche kivulini mwa mabawa yako,*
mbali na mashambulio ya waovu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Adui wa hatari wanizunguka,/
hawana huruma yoyote ile;*
wamejaa maneno ya kujigamba.

Sasa wamenizingira pande zote;*
wanavizia waniangushe chini.

Wako tayari kunirarua kama simba;*
kama aviziavyo mawindo mwana-simba.

Uje, Ee Mungu, kuwakabili na kuwaporomosha.*
Kwa upanga wako uniokoe na watu waovu;

kwa mkono wako, Ee Mungu, uniokoe na watu hao,*
watu ambao huthamini riziki ya dunia hii tu.

Waadhibu kwa mateso uliyowawekea,/
yawe ya kutosha kwa watoto wao,*
wawaachie na wajukuu wao.

Lakini mimi nitakuona, kwani sikutenda ubaya;*
niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Baba, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nimewatuma hao ulimwenguni (aleluya).

Adhuhuri
Ant.: Mtu anayewapokea ninyi, hunipokea mimi: yeyote anayenipokea mimi, humpokea Yeye aliyenituma (aleluya).

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Sisi twafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni bustani ya Mungu, ni jengo la Mungu (aleluya).

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Tim.4:16
Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo, maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.

K. Bwana alimchagua mtumishi wake (aleluya).
W. Alimwita awe mchungaji wa Yakobo, urithi wake (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Tim.1:12
Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo, aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie.

K. Sitaona aibu kutangaza Habari Njema (aleluya).
W. Uwezo wa Mungu ndio unaowaokoa watu (aleluya).

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Tim.3:13
Wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu.

K. Kama Bwana haijengi nyumba hiyo (aleluya).
W. Wale waijengao wafanya kazi bure (aleluya).

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulifanye upya Kanisa lako kwa Roho yule wa hekima na upendo uliyemjalia kikamilifu Mtakatifu Augustino. Utuongoze kwa Roho huyo huyo ili tukutafute wewe, uliye pekee chemchemi ya hekima ya kweli, na chanzo cha upendo wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.