Generic placeholder image

Agosti 29
KUKATWA KICHWA YOHANE MBATIZAJI
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Mungu aliwaita manabii,
Manabii walio maarufu,
Wabashiri wa Mwanae ujio;
Mkuu kabisa kati ya hao,
Kabla ya kuzaliwa kaitwa,
Alikuwa Yohane, mteule.

Yohane, katika upweke wake,
Alimtafuta sana Kristo,
Akamtambua alipokuja;
Ndipo walimwengu kawaonesha
Mwana-Kondoo wa Mungu wamwone;
Akamsalimu badala yetu.

Na ile sauti pweke nyikani
Ukweli hasa ilipotangaza
Ilipuuzwa na kukataliwa.
Na kwa dhati alipoitetea
Sheria ya Mungu kusisitiza,
Kifodini kamfika Yohane.

Basi sisi tunakusifu Wewe
Uliye Utatu, Mungu Mmoja,
Nuru iangazayo kwenye giza,
Ndiwe tumaini la watu wote
Ambao wanakutafuta sana
Wewe utupendaye siku zote.

ANT. I: Usiwaogope hao, maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana.

Zab.116:1-9 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.

Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.

Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.

Kisha nikamlilia Mungu:*
“Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!“

Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.

Mungu huwalinda wanyofu;*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.

Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.

Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.

Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Usiwaogope hao, maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana.

ANT. II: Herode alimtuma mmoja wa askari wake kumkata kichwa Yohane, ambaye alikuwa gerezani.

Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Nilizidi kuamini hata niliposema:*
"Mimi naangamia."

Hata niliposema kwa hofu;*
"Binadamu hawaaminiki."

Nimrudishie Mungu nini,*
kwa mema yote aliyonitendea?

Nitamtolea Mungu dhabihu ya kinywaji,*
nimheshimu kwa shukrani.

Nitamtimizia Mungu nadhiri zangu,*
mbele ya taifa lake lote.

Mungu huthamini kifo cha waaminifu wake.*
Ee Mungu, mimi ni mtumishi wako;

ni mtumishi wako kama alivyokuwa mama yangu;*
umeniweka huru.

Nitakutolea sadaka za shukrani,*
na kukupa heshima zangu.

Mbele ya taifa lako lote,/
ukumbini mwa Hekalu lako huko Yerusalemu,*
nitakutimizia yale niliyoahidi, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Herode alimtuma mmoja wa askari wake kumkata kichwa Yohane, ambaye alikuwa gerezani.

ANT. III: Wanafunzi wa Yohane wakaenda na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwana-kondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Wanafunzi wa Yohane wakaenda na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

SOMO: Mate.13:23-25
Kutokana na ukoo wake Daudi, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mkombozi, ndiye Yesu. Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa. Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake, aliwaambia watu: 'Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu, na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake."

KIITIKIZANO
K. Rafiki ya bwana arusi, hufurahi anapoisikia sauti ya bwana arusi. (W. Warudie)
K. Sasa furaha yangu imekamilika.
W. Maana nimeisikia sauti ya bwana arusi.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Rafiki...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mimi siye Kristo, bali ni mtangulizi wake. Yeye ni lazima azidi kuwa maarufu, na mimi ni lazima nipungue.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mimi siye Kristo, bali ni mtangulizi wake. Yeye ni lazima azidi kuwa maarufu, na mimi ni lazima nipungue.

MAOMBI
Mungu Baba yetu, ulimchagua Yohane Mbatizaji kwa ajili ya kuwatangazia watu wote utawala wa Kristo. Kwa hiyo tunasali kwa furaha.
W. Bwana, utuongoze katika njia ya amani.

Ulimchagua Yohane kabla hajazaliwa, ili apate kumtayarishia njia Mwanao:
- utujalie imani ya kumjua Kristo, na ya kumtangaza kwa wengine. (W.)

Ulimwongoza Yohane Mbatizaji, hata akamtambua Mwana-Kondoo wa Mungu;
- kwa njia yetu uuwezeshe ulimwengu kumtambua Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo. (W.)

Ulimwelekeza nabii wako amwachie nafasi Kristo;
- utupatie unyenyekevu, tuweze kuruhusu nuru yake ing'ae ulimwenguni. (W.)

Ulimtaka Yohane afanye kazi yako, hata auawe kwa ajili yako:
- utujalie tuweze kushiriki ari yake ya kutangaza ukweli. (W.)

Uwakumbuke marehemu:
- uwafikishe kwenye maisha mapya, wakiwa wametakaswa na kila doa la dhambi. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Baba yetu, ulimteua Mtakatifu Yohane Mbatizaji awe mtangulizi wa kuzaliwa na wa kufa kwa Kristo Mwanao. Utujalie tuweze kulishuhudia neno lako kishujaa kama yeye alivyofanya, hata akauawa kwa ajili ya kutetea haki na ukweli. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.