Tarehe 14 Septemba

KUTUKUKA KWA MSALABA
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Gal.6:14
Lakini sisi yatupasa kuona fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ndani yake mna wokovu, uzima na ufufuko wetu, nasi tumepata kuokolewa na kukombolewa naye.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Mungu, ulitaka Mwanao pekee ateswe msalabani ili kuwaokoa wanadamu. Tunakuomba utujalie sisi tuliojua fumbo lake hapa duniani tustahili kupata thawabu ya ukombozi wake huko mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutwala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hes.21:4-9
Siku zile jangwani, watu walimnung’unikia Mungu, na Musa, mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unukia Mungu, na wewe, utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.78:1-2,34-38(K)7
1. Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu,
Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.
Na nifunue kinywa changu kwa mithali,
Niyatamke mafumbo ya kale.

(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.

2. Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta;
Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.
Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao,
Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wako. (K)

3. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao,
Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.
Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake,
Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. (K)

4. Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema,
Husamehe uovu wala haangamizi.
Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake,
Wala haiwashi hasira yake yote. (K)

SOMO 2: Fil.2:6-11
Yesu Kristo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama wanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Ee Kristu tunakuabudu na kukutukuza, kwa kuwa umeikomboa dunia kwa msalaba wako.
Aleluya!

INJILI: Yn.3:13-17
Yesu alimwambia Nikodemo: Hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba sadaka hii itutakase maovu yetu yote, sadaka ambayo iliondoa maovu ya ulimwengu mzima katika altare ya msalaba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI
Ushindi wa Msalaba mtukufu.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe ulileta wokovu wa watu katika mti wa msalaba, ili pale mauti yalipoanzia, palepale pawe chanzo cha uzima; na yule mwovu aliyeshinda zamani katika mti, katika mti pia ashindwe kwa njia ya Kristo, Bwana wetu.
Kwa njia yake Malaika husifu adhama yako, Enzi hukuabudu, na Mamlaka hukupigia magoti wakitetemeka. Mbingu na Nguvu za mbinguni, na Maserafi wenye heri, wakuadhimisha pamoja kwa shangwe.
Tunakusihi, utujalie tujiunge nao kwa wimbo wa sifa, tukisema kwa sauti ya unyenyekevu:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ...

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn12:32
Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu, asema Bwana.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana Yesu Kristo, baada ya kulishwa kwa sakramenti yako takatifu, tunakuomba kwa unyenyekevu, sisi uliotukomboa kwa mti wa msalaba utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Unayeishi na kutawala milele na milele.