MT. MATAYO MTUME NA MWINJILI
MASOMO
SOMO: Efe.4:1-7,11-13
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;
kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi
kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani, mwili mmoja, na Roho mmoja, Imani moja,
ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani
ya yote. Lakini kila mmoja wenu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.
Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na
wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma
itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa Imani na
kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha
utimilifu wa Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:1-4(K)4
1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya!
INJILI: Mt.9:9-13
Yesu alipokuwa akipita aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate.
Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na
wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona,
waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye
dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.
Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana
sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.