Tarehe 01, Oktoba

MT. TERESA WA MTOTO YESU BIKIRA NA MWALIMU WA KANISA
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Kum.32:10-12
Bwana alimzunguka, akamtunza, akamhifadhi kama mboni ya jicho. Mfano wa tai alikunjua mbawa zake, akamtwaa, akamchukua juu ya mbawa zake. Bwana peke yake alimwongoza.

KOLEKTA:
Ee Mungu, unawapatia ufalme wako wanyenyekevu na watoto wadogo. Utufanye tufuate kiaminifu nyayo za mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu, bikira, ili, kwa maombezi yake, tufunuliwe utukufu wako wa milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO: Rum.8:26-30
Ndugu zangu, Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachangua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.131
1. Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijishughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu.

(K) Ee Bwana, uilinde nafsi yangu katika amani yako.

2. Hakika nimeituliza nafsi yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa,
Kifuani mwa mama yake,
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu. (K)

SHANGILIO: Mt.5:8
Aleluya, aleluya!
Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.
Aleluya!

INJILI: Mt.18:1-4
Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, katika mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu, sisi tunatangaza kuwa wewe ni wa ajabu. Tunakuomba kwa unyenyekevu wewe mtukufu, ili, kama vile ulivyopendezwa na mastahili yake, hali kadhalika yakupendeze matendo ya utumishi wetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.18:3
Bwana asema: Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti tuliyoipokea iwashe ndani mwetu moto wa upendo uliomfanya mtakatifu Teresa ajiachilie mwenyewe kwako, na atamani kuwaombea Watu wote huruma yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.