MALAIKA WALINZI
MASOMO
SOMO: Kut.23:20-23
Bwana asema hivi: Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka
mpaka mahali pale nilipokutengenezea. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani;
maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini ukiisikiza sauti yake
kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao
wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti,
na Mpezi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.91:1-6.10-11(K)11
1. Aketiye mahali pa siri pake aliye juu,
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu nitakayemtumaini.
(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.
2. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
Na katika tauni iharibuyo.
Kwa manyoya yake atakufunika,
Chini ya mbawa zake utapata kimbilio. (K)
3. Hutaogopa hofu ya usiku,
Wala mshale urukao mchana,
Wala tauni ipitayo gizani.
Wala uele uharibuo adhuhuri, (K)
4. Mabaya hayatakupata wewe,
Wala tauni haitaikaribia hema yako.
Kwa kuwa atakuagizia malaika zake
Wakulinde katika njia zako zote. (K)
SHANGILIO: Mt.18:1-5,10
Aleluya, aleluya!
Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
Aleluya!
INJILI: Mt.18:1-5.10
Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita
mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto,
hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu,
huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu
kwa jina langu, anipokea mimi. Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya
kwamba malaika zao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.