Generic placeholder image

Oktoba 2
MALAIKA WALINZI
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Waja, wajumbe wa Mungu,
Matarishi wa upendo,
Waja kutoka milki
Za amani zilo juu,
Kutoka makazi bora
Ya nuru isofifia,
'Toka majumba ya raha
Na furaha ya daima.

Waja kutulinda sisi
Hapa tulipo mahali,
Kutufariji ta'buni,
Tutuliza mashakani:
Viongozi wa mbinguni
Msitukimbie sisi,
Mungu anataka ninyi
Daima mkae nasi.

Ila kazi yenu hasa
Ni roho kusaidia
Inapofikia mwisho
Wa safari yake hiyo,
Na kuunong'onezea
Moyo ambao wataka:
'Ewe roho ya Kikristo,
Uondoke kwa amani.'

Bidii utupatie
Na ari ya malaika,
Ili tukutumikie
Kwa upendo maishani;
Utupatie twasihi
Na Malaika - mlinzi
Katika mahangaiko
Ya saa ya kufa kwetu.

ANT. I: Malaika wa Bwana hupiga kambi kuwazunguka wale wamchao Bwana, ili awaokoe.

Zab.34 Sifa kwa wema wa Mungu
I

Nitamtukuza Mungu nyakati zote,*
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.

Nitamwonea Mungu fahari,*
wanaodhulumiwa wasikie na wafurahi.

Mtukuzeni Mungu pamoja nami,*
sote pamoja tulisifu jina lake.

Nilimwomba Mungu, naye akanisikiliza,*
akaniondolea hofu zangu zote.

Mgeukieni Mungu, mpate kufurahi;*
hamtapata kamwe kuaibika.

Maskini alimlilia Mungu, naye akamsikiliza,*
na kumwokoa katika shida zake zote.

Malaika wa Mungu huwalinda wote wamchao,*
na kuwaokoa katika hatari.

Jioneeni wenyewe jinsi Mungu alivyo mwema.*
Heri wanaokimbilia usalama kwake.

Mcheni Mungu, enyi watakatifu wake;*
wenye kumcha hawakosi mahitaji yao.

Hata simba huona njaa kwa kutindikiwa;*
bali wanaomtii Mungu wana kila kitu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Malaika wa Bwana hupiga kambi kuwazunguka wale wamchao Bwana, ili awaokoe.

ANT. II: Kama Mungu aishivyo, vivyo hivyo malaika wake amenilinda.

II
Njoni, enyi vijana, mkanisikilize,*
nami nitawafundisheni kumcha Mungu.

Je, wapenda kufurahia maisha;*
kuishi maisha marefu na ya fanaka?

Basi, acha kusema mabaya;*
achana na hila.

Jiepushe na uovu, utende mema;*
tafuta amani na kuizingatia.

Mungu huwaangalia waadilifu,*
na kusikiliza malalamiko yao;

lakini huwapinga watendao mabaya,*
awaondoa duniani, wasahauliwa kabisa.

Waadilifu wakimlilia Mungu, huwasikiliza,*
na kuwaokoa katika taabu zao zote.

Mungu yu karibu na waliovunjika moyo;*
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.

Mateso ya mwadilifu ni mengi,*
lakini Mungu humwokoa katika yote.

Ubaya utawaangamiza watu waovu;*
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.

Mungu humlinda mtu mwadilifu,*
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.

Mungu atawaokoa watu wake,*
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Kama Mungu aishivyo, vivyo hivyo malaika wake amenilinda.

ANT. III: Mshukuruni Mungu wa mbingu, pamoja na viumbe vyote mtukuzeni yeye, maana amewaonesheni fadhili zake kuu.

WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-12a
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!

Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!

Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.

Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,

watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.

Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu

akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.

Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!

Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwana-kondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;

Kwa sababu hiyo furahini, enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.

maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Mshukuruni Mungu wa mbingu, pamoja na viumbe vyote mtukuzeni yeye, maana amewaonesheni fadhili zake kuu.

SOMO: Ufu.8:3-4
Malaika mwingine akafika, akiwa amechukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya altare ya kuteketezea ubani. Naye akapewa ubani mwingi, autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu, juu ya altare ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi. Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.

KIITIKIZANO
K. Mungu amewakabidhi kwa malaika wake, ili wawatunze. (W. Warudie)
K. Basi, na wawalinde ko kote mwendako.
W. Ili wawatunze.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mungu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Daima malaika wanaukazia macho, uso wa Baba yangu mbinguni.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Daima malaika wanaukazia macho, uso wa Baba yangu mbinguni.

MAOMBI
Baba yetu, atuweke tayari kutekeleza matakwa yake hapa duniani.
W. Pamoja na majeshi ya mbinguni, tumsifu Baba.

Bwana, uliwaumba malaika ili wawe wahudumu wa neno lako:
- kwa msaada wao, tufanikiwe kuwapelekea ndugu zetu neno lako. (W.)

Bwana, utakatifu wako unaimbwa na malaika wa milele:
- Kanisa duniani kamwe lisishindwe kukusifu. (W.)

Uliwatuma malaika wako kuwaangalia watumishi wako,
- uwalinde wote wanaosafiri, na uwafikishe nyumbani salama. (W.)

Siku ya Noeli, malaika wako waliimba: amani waipate wanadamu;
- ujumbe wao wa amani uamshe na kuchochea mioyo ya watawala na raia. (W.)

Malaika watakapowakusanya marehemu kutoka pembe nne za dunia,
- watu wako wakusanywe pamoja, na kuingizwa katika furaha yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu wa majeshi, kwa maongozi yako ya busara, uliwatuma malaika ili watutunze na kutulinda sisi. Utuzungushie ulinzi wao hapa duniani, na utupatie furaha ya kujumuika nao milele mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.