Generic placeholder image

Oktoba 2
MALAIKA WALINZI
JUMATANO JUMA LA 26 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT. I: Nimezitafakari njia zangu, na nimeyarudia mapenzi yako.

Zab.119:57-64 VIII Heshima kwa sheria ya Mungu
Ee Mungu, ndiwe uliye pekee muhimu kwangu;*
naahidi kushika maagizo yako.

Nakusihi kwa moyo wangu wote;*
unionee huruma kama ulivyoahidi!

Nimeufikiria mwenendo wangu,*
na ninaahidi kuyafuata maagizo yako.

Bila kukawia nafanya haraka*
kuzishika amri zako.

Ingawa mitego ya wakosefu inanisonga,*
lakini sisahau sheria yako.

Usiku wa manane naamka kukusifu,*
kwa sababu ya hukumu zako adilifu.

Mimi ni rafiki ya wote wakuchao,*
wa wote wanaozitii amri zako.

Dunia imejaa upendo wako mkuu, Ee Mungu;*
unifundishe kanuni zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nimezitafakari njia zangu, na nimeyarudia mapenzi yako.

ANT. II: Hofu na tetemeko limenijia; unielekee na kusikiliza kilio changu, Ee Bwana.

Zab.55:1-14,16-23 Sala ya mtu anayedhulumiwa
Yesu akaanza kufadhaika sana na kuhangaika (Mt.14:33)

I
Ee Mungu, sikiliza sala yangu;*
usilipe kisogo ombi langu.

Unisikilize na kunikubalia;*
nimechoshwa na mahangaiko yangu.

Nina hofu kubwa kwa vitisho vya adui zangu,*
na kwa kudhulumiwa na watu waovu.

Watu waovu wananitaabisha,*
na kwa hasira wananifanyia uhasama.

Moyo wangu umejaa hofu,*
vitisho vya kifo vimenisonga.

Natetemeka kwa hofu kubwa,*
nimevamiwa na vitisho vikubwa.

Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa!*
Ningeruka mbali na kupata pumziko;

naam, ningesafiri mbali sana,*
na kupata makao jangwani.

Ningekimbilia mahali pa usalama,*
mbali na upepo mkali na dhoruba.

Ee Bwana, vuruga lugha yao;*
maana naona ukatili na ugomvi mjini,

vikiuzunguka usiku na mchana,*
na kuujaza maafa na jinai.

Uharibifu umeenea pote mjini,*
uhasama na ukandamizaji kila mahali.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Hofu na tetemeko limenijia; unielekee nakusikiliza kilio changu, Ee Bwana.

ANT. III: Nitamlilia Mungu, naye Bwana ataniokoa.

II
Kama adui yangu angenitukana,*
ningeweza kustahimili hayo;

kama mpinzani wangu angenidharau,*
ningeweza kujificha mbali naye.

Kumbe, lakini, ni wewe mwenzangu;*
ni wewe rafiki yangu na msiri wangu!

Sisi tulizoea kuzungumza kirafiki;*
pamoja tulifanya ibada nyumbani mwa Mungu.

Lakini mimi namlilia Mungu,*
naye Mungu ataniokoa.

Jioni, asubuhi na adhuhuri,/
nalalama na kulia kwa huzuni,*
naye ataisikia sauti yangu.

Ataniokoa na kunisalimisha*
katika vita ninavyovikabili, dhidi ya maadui wengi.

Mungu atawalaye tangu milele,/
atatega sikio na kuwashinda;*
maana hawashiki sheria wala kumcha Mungu.

Mwenzangu amewashambulia rafiki zake,*
amevunja mapatano yake.

Maneno yake laini kuliko siagi,*
lakini moyo wake watamani vita.

Maneno yake mororo kama mafuta,*
lakini yanakata kama upanga mkali.

Mwachie Mungu mzigo wako,/
naye atakutegemeza;*
kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.

Lakini wauaji na wabaya,*
Mungu atawaporomosha shimoni mwa maangamizi,

kabla ya kufikia nusu ya maisha yao.*
Lakini mimi nitakutumainia wewe, Ee Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Nitamlilia Mungu, naye Bwana ataniokoa.

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Mate.5:17-20
Kisha, Kuhani Mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Wasadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu. Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu. Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia, "Nendeni mkasimame Hekaluni, na kuwaambia watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya."

K. Nitakuimbia, Mungu wangu, mbele ya malaika.
W. Tutakuabudu hekaluni mwako, na kutoa ushuhuda juu ya jina lako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Mate.12:7
Ghafula malaika wa Bwana akasimama karibu naye, na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa akisema, "Amka upesi!" Mara ile minyororo ikaanguka kutoka katika mikono yake.

K. Bwana alimtuma malaika wake.
W. Ambaye aliniokoa kutoka katika mikono ya Herode.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Mate.10:3-5
Yapata saa tisa mchana, aliona dhahiri katika ono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, "Kornelio!" Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, "Kuna nini, Mheshimiwa?" Huyo malaika akamwambia, "Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini. Sasa, watume watu Yopa, wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine, Petro."

K. Moshi wa ubani unukiao, wa sala za watakatifu, ulipaa mbele ya Bwana.
W. Ulipaa mbele ya macho ya Mungu, kutoka katika mkono wa malaika.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu wa majeshi, kwa maongozi yako ya busara, uliwatuma malaika ili watutunze na kutulinda sisi. Utuzungushie ulinzi wao hapa duniani, na utupatie furaha ya kujumuika nao milele mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.