Generic placeholder image

Oktoba 7
MAMA YETU WA ROZARI
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo ni Mwana wa Maria: njooni, tumwabudu (aleluya).

Au:
Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha, tunapomheshimu Bikira Maria Mwenye heri (aleluya).

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Maria mwenye taji ya nuru
Wewe ni hekalu lake Bwana,
La amani na utakatifu,
Ndiwe nyumba akaamo neno.

Fumbo la maisha bila dhambi
Kati ya watu walopotoka;
Kivuli wewe huna, wang'aa,
Sababu una neema tele.

Bikira Mama wa Mungu wetu,
Utuinue tuangukapo,
Umekuwa mama yetu sote,
Kasema Yesu Msalabani.

Baba, Mwana pamoja na Roho,
Mbingu masifu zawaimbia;
Anawatukuzeni Maria,
Siku zote na hata milele.

ANT. I: Yesu, aitwaye Kristo, ni Mwana wa Maria.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Yesu, aitwaye Kristo, ni Mwana wa Maria.

ANT. II: Pamoja nawe, Mama yetu, tunatoa shukrani kwa Bwana; Yeye alipokuwa anakufa, alitukabidhi kwako ututunze.

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Pamoja nawe, Mama yetu, tunatoa shukrani kwa Bwana; Yeye alipokuwa anakufa, alitukabidhi kwako ututunze.

ANT. III: Bikira Maria amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika; kichwani amevikwa taji ya nyota kumi na mbili.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Bikira Maria amekwezwa juu zaidi kuliko makundi ya malaika; kichwani amevikwa taji ya nyota kumi na mbili.

SOMO: Isa.61:10
Nilifurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.

KIITIKIZANO
K. Salamu, Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe. (W. Warudie)
K. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na yeye. utakayemzaa amebarikiwa.
W. Bwana yu nawe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Salamu...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Mama mwenye heri, na Bikira safi, malkia mtukufu wa ulimwengu, tunaomba wote wanaoadhimisha sikukuu yako, waweze kuona nguvu ya maombezi yako.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mama mwenye heri, na Bikira safi, malkia mtukufu wa ulimwengu, tunaomba wote wanaoadhimisha sikukuu yako, waweze kuona nguvu ya maombezi yako.

MAOMBI
Tutangaze ukuu wa Mwokozi wetu, aliyechagua kuzaliwa na Bikira Maria. Tukitumaini kwamba atatusikiliza, tuombe:
W. Bwana, mama yako atuombee.

Mwokozi wa ulimwengu, kwa nguvu yako ya kukomboa, ulimkinga mama yako na kila doa la dhambi;
- utuopoe kutoka katika uovu uliojificha mioyoni mwetu. (W.)

Kristo, Mkombozi wetu, ulimfanya Bikira Maria awe makao yako, na awe hekalu la Roho;
- utufanye tuwe makao ya Roho wako. (W.)

Neno wa milele, ulimfundisha mama yako Maria kuchagua kilicho bora kabisa;
- utuwezeshe kufuata mfano wake, na kutafuta kwa bidii chakula kiletacho uzima wa milele. (W.)

Mfalme wa wafalme, ulimpaliza Maria mbinguni, ili awe pamoja nawe, mwili na roho;
- utuwezeshe kuyatafuta yaliyo ya juu, na kuyaelekeza maisha yetu kwako. (W.)

Mfalme wa mbingu na dunia, ulimketisha Mama Maria karibu nawe, ili awe malkia, atawale milele;
- utujalie furaha ya kushiriki utukufu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, uifungue mioyo yetu ipate kuingiza neema yako. Sisi ambao tumejifunza kusadiki kutokana na taarifa ya malaika - kwamba Kristo Mwanao alikuwa mwanadamu, kwa mateso yake na msalaba wake, na kwa maombezi ya Bikira Maria Mwenye Heri, tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.