Generic placeholder image

Oktoba 7
MAMA YETU WA ROZARI
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bikira, na papo hapo ni Mama,
Binti yake Mwana wako mwenyewe,
U juu kuliko wengine wote
Ila hapana wa chini zaidi;
Wewe ndio utimilifu wote
Ulopangwa kwa amri ya Mungu
Ulimwengu wetu uloanguka
Katika wewe lipokuwa bora!

Akisha tayarishiwa mahali,
Yeye aliyeumba vitu vyote
Kakaa kati ya viumbe vyake,
Kifuani pako ndo akalala;
Hapo akalisha upendo wake
Kwa joto ambalo liliukuza
Mzizi ule ulostawisha
Amani yetu sisi ya milele.

Na si peke yako usikiaye
Sisi tunaposifu lako jina;
Mara nyingi huwa karibu sana
Sauti zetu zinapokatika;
Viumbe vyote kaumbwa vizuri
Kwa umbo na kwa sura yako nzuri,
Huruma, nguvu, upole na wema,
Na neema umejaliwa mama.

Bibi, tushindwapo kuona mbele,
Katika kutarajia ya mbingu,
Endelea bado kutuombea
Sisi kwa huyo Mwanao daima,
Ambaye anastahili sifa,
Nguvu na enzi na wote uweza,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Na pamoja na Baba mtukufu.

ANT. I: Malaika Gabrieli alimpasha Maria habari njema, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Malaika Gabrieli alimpasha Maria habari njema, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

ANT. II: Mama ya Yesu alisimama karibu na msalaba.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Mama ya Yesu alisimama karibu na msalaba.

ANT. III: Furahi, Ee Mama Bikira; Kristo amefufuka kutoka kaburini, aleluya.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Furahi, Ee Mama Bikira; Kristo amefufuka kutoka kaburini, aleluya.

SOMO: Gal.4:4-5
Wakati ule maalum ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria, apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria, ili sisi tufanywe wana wa Mungu.

KIITIKIZANO
K. Salamu Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe. (W. Warudie)
K. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mzao wako amebarikiwa.
W. Bwana yu nawe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Salamu...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Maria aliyaweka maneno hayo yote moyoni mwake, akayatafakari.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Maria aliyaweka maneno hayo yote moyoni mwake, akayatafakari.

MAOMBI
Tumtukuze Mungu Baba, aliyemchagua Maria awe mama ya Mwanae, na aliyetaka vizazi vyote vimwite ni mwenye heri. Kwa imani na matumaini, tuombe:
W. Maria Mtakatifu utuombee.

Baba, umemwangalia kwa huruma Bikira Maria, na umemfanya awe mama wa huruma;
- watu walio katika hatari, waonje upendo wake mkuu. (W.)

Ulimchagua Maria awe mama katika nyumba ya Yosefu;
- kwa sala zake, uwasaidie akina mama wote kuzifanya nyumba zao ziwe makao ya upendo na utakatifu. (W.)

Ulimjalia Mama Maria nguvu ya kusimama chini ya msalaba, na kwa ufufuko ukamfurahisha na kumliwaza;
- uwainue wenye huzuni na uyafanye maisha yao yawe na matumaini. (W.)

Maria alikuwa mtumishi wako mwaminifu, ambaye aliyaweka maneno yako moyoni mwake;
- kwa maombezi yake, utuwezeshe kuwa wanafunzi wa kweli wa Mwanao, tuliojitoa mhanga kumtumikia yeye. (W.)

Baba, ulimtukuza Bikira Maria, na kumfanya awe Malkia wa mbingu;
- uwajalie marehemu kuingia katika ufalme wako, na kufurahi pamoja na watakatifu wako milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, uifungue mioyo yetu ipate kuingiza neema yako. Sisi ambao tumejifunza kusadiki kutokana na taarifa ya malaika - kwamba Kristo Mwanao alikuwa mwanadamu, kwa mateso yake na msalaba wake, na kwa maombezi ya Bikira Maria Mwenye Heri, tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.