Tarehe 18, Oktoba

MT. LUKA MWINJILI
MASOMO

SOMO: 2Tim.4:10-17
Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi. Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso. Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi. Iskanda, mfua shaba, alionesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake. Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu. Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:10-13,17-18(K)12
1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi,
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.

(K) Wacha wako, Ee Bwana, wajulisha matendo yako makuu na utukufu wa fahari ya ufalme wako.

2. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)

SHANGILIO: Yn.15:1-9
Aleluya, aleluya!
Ni mimi niliyewachagua ninyi, nikawaweka mwende mkazae matunda, matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya!

INJILI: Lk.10:1-9
Bwana aliweka wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni; angalieni, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwa mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni Ufalme wa Mungu umewakaribia.