NOVEMBA 1
WATAKATIFU WOTE

MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA
Tufurahi sote katika Bwana tunapoadhimisha sikukuu kwa heshima ya watakatifu wote; Malaika nao wanaishangilia sikukuu hii na kumhimidi Mwana wa Mungu.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, umetujalia kuadhimisha kwa sherehe moja mastahili ya watakatifu wako wote. Tunakuomba, kwa msaada wa hao waombezi wengi, utukirimie wingi wa huruma yako unaotamaniwa. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Ufu.7:2-4,9-14
Mimi Yohane, niliona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri wa Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwanakondoo wamevikwa mavazi meupe wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwanakondoo. Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai Wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu, wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je, watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6(K)6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)

3. Atapokea baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako,Ee Mungu wa Yakobo.(K)

SOMO 2: 1Yoh.3:1-3
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo! Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.

SHANGILIO: Mt.11:28
Aleluya, aleluya!
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao
na wenye kulemewa na mizigo,
nami nitawapumzisha, asema Bwana.
Aleluya!

INJILI: Mt.5:1-12
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafuzi Wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
Heri walio maskini wa roho;
Maana ufalme wa mbinguni ni wao
Heri wenye huzuni;
Maana hao watafarijika.
Heri wenye upole;
Maana hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu ya haki;
Maana hao watashibishwa
Heri wenye rehema;
Maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi;
Maana hao watamwona Mungu.
Heri wapatanishi;
Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki;
Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Wakristo wenzangu, Mungu alitaka kutuunganisha wote tuishi kama familia kubwa mbinguni. Wengine walitangulia kukaribishwa katika makao ya milele. Wanatuombea tupate neema ya kujiunga nao. Kwa maombezi ya watakatifu Tuombe. Ee Mungu unayetuandalia makao ya milele na Watakatifu wako,

1. Ulitupelekea watakatifu watuoneshe njia ya kufika mbinguni: Utuangaze tufuate mfano wao.

2. Watakatifu walikupenda zaidi ya yote duniani: Utupe neema hii ya kukutii Wewe na kukupa mahali pa kwanza katika maisha yetu.

3. Utuhimize tuoneshe imani ya kweli kwa matendo ya upole, huruma na upendo.

4. Utupe moyo wa kukukiri na kukushuhudia mbele ya watu wote bila woga.

5. Utufanye sisi kuwa waumini halisi ili tuwavute wengine wakupende kama sisi tunavyojaribu kukupenda.

6. Uwapokee waumini wote marehemu katika ushirika wa watakatifu.

Ee Mungu Mwenyezi, wewe u Mungu wa upendo. Kwa hiyo umeazimia kuwashirikisha viumbe vyako katika heri yako ya milele, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, vipaji vyetu tunavyokutolea kwa heshima ya watakatifu wote vikupendeze. Tunakuomba utujalie ili tutambue kwamba wanashughulikia wokovu wetu, hao tunaosadiki kwamba wamekwisha kupata uzima wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Utukufu wa mama yetu Yerusalemu
K.
Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Maana leo unatujalia kuutukuza mji wako, Yerusalemu ya mbinguni, ambao ni mama yetu. Huko ndugu zetu watakatifu wanakuzunguka na kukusifu milele. Nasi pia tunaukaribia kwa imani mji huo kama wasafiri.
Tunakwenda hima tukiufurahia kwa pamoja utukufu mkuu uliowapa wanakanisa. Kwa kuwatukuza hivyo unatujalia wawe misaada na mifano katika udhaifu wetu.
Na kwa sababu hiyo, sisi pamoja na umati mkuu wa watakatifu na malaika tunakutukuza kwa sauti moja tukisema.

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.5.8-10
Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu; heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu; heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu, tunakuabudu wewe uliye peke yako mtakatifu na wa ajabu katika watakatifu wako wote. Tunakuomba neema yako, ili, kwa kututakatifuza kikamilifu katika utimilifu wa upendo wako, ituwezeshe kuvuka kutoka meza hii ya wasafiri hadi kuifikia karamu ya kwetu mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.