NOVEMBA 2
MAREHEMU WOTE

Misa ya kwanza

ANTIFONA YA KUINGIA (IThe 4:14; 1Kor 15:22)
Kama vile Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.

KOLEKTA:
Ee Bwana, tunakuomba usikilize kwa wema sala zetu, ili, kama vile imani yetu katika Mwanao mfufuka kutoka wafu inavyoimarishwa, vivyo hivo tumaini letu la kutazamia ufufuko wa watumishi wako lithibitishwe. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Ayu 19:1, 23-27
Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Yakachorwa katika mwamba milele, Kwa kalamu ya chuma na risasi. Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu!

WIMBO WA KATIKATI: Zab 27:1, 4, 7-9, 13 (K) I au 13
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?

(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
au: Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai.

2. Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)

3. Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia,
Unifadhili, unijibu.
Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako. (K)

4. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

SOMO 2: Rum. 5:5-11
Tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika miyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonesha pendo lake kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo utapanisho.

SHANGILIO: Yn 6:40
Aleluya, aleluya!
Mapenzi yake Baba yangu ni haya, asema Bwana, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
Aleluya!

INJILI: Yn 6:37-40
Siku ile Yesu aliwaambia watu wote waliokuwapo: Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapezi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu mi haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

MAOMBI
Ndugu zangu, Bwana Yesu alisema hivi: Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi. Ninakwenda kuwaandalia makao ili nikija niwachukue mpate kuwapo nilipo mimi. Ee Mungu Mwenyezi,

1. Uwakaribishe marehemu walioaga dunia katika makao ya milele.

2. Uwatulize marehemu walioteswa na kuhuzunishwa katika bonde la machozi la hapa duniani.

3. Uwapokee katika makao ya milele marehemu wale wote waliouawa duniani, waliofukuzwa kwao na katika nchi zao na kusahauliwa na ndugu na jamaa zao.

4. Uwakusanye watoto wote walionyimwa maisha duniani kwa kuuawa katika utoaji mimba.

5. Uamshe ndani yetu sisi tulio bado hai duniani matumaini ya kukaribishwa nawe mbinguni.

6. Utusaidie kupokea kifo kama sehemu ya maisha yetu.

Ee Baba, Bwana wa makao ya milele, tunakuletea maombi yetu kwa njia ya Mwanao Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vyetu, ili watumishi wako marehemu wapokelewe katika utukufu pamoja na Mwanao, ambaye, kwa njia ya sakramenti yake kuu ya upendo wote tunaunganishwa naye. Anayeishi na kutawala milele na milele

UTANGULIZI wa wafu

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn 11:25-26
Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima, asema Bwana. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, tumeadhimisha sakramenti ya Pasaka kwa ajili ya watumishi wako marehemu. Tunakuomba, uwajalie waingie katika makao ya mwanga na amani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.