Tarehe 9 Novemba

SIKUKUU YA
KUTABARUKIWA KANISA LA LATERANI

MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA:
Niliona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Nao ulikuwa umetayarishwa kama bibi harusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

KOLEKTA:
Ee Mungu, kwa mawe hai na mateule, wewe unatayarisha makao yako ya milele kwa ajili ya adhama yako. Uzidishe katika Kanisa lako neema uliyolijalia, ili waamini wako waongezeke daima katika ujenzi wa Yerusalemu ya mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 1Fal.8:22-23,27-30
Wakati ule, Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni. Akasema, "Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini! Ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote. Lakini Mungu je atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga! walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako. Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu'; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo, akikabili mahali hapa. Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.”

WIMBO WA KATIKATI: Zab.95:1-2,6-9, (K) 8
1. Njoni tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.

(K) Tumwabudu Mungu katika nyumba yake takatifu!

2. Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Mkononi mwake zimo bonde za dunia,
hata vilele vya milima ni vyake.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya,
na mikono yake iliumba nchi kavu. (K)

3. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

SOMO 2: 1Pet.2:4-9
Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko, Tazama, naweka katika Sayuni Jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, na kila amwaminiye hatatahayarika. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha. Kwa maana hujikwaza kwa neno lile, wasiliamini, nao waliwekwa kusudi wapate hayo. Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

SHANGILIO: Mk.11:17
Aleluya, aleluya!
Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Yn.4:19-24
Siku ile yule mwanamke Msamaria alimwambia Yesu, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwambudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uvipokee vipaji hivi vilivyotolewa kwako, na uwajalie wale wakuombao humu wapokee nguvu ya sakramenti hii na matunda ya sala zao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: fumbo la kanisa, bibi harusi wa Kristo na hekalu la Roho.
K.
Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe, kwa wema wako umekubali kukaa katika nyumba ya sala, ili sisi tunaotegemezwa daima kwa msaada wa neema yako, tufanywe hekalu la Roho Mtakatifu na tung'ae katika uangavu wa maisha yanayokupendeza.
Majengo haya ni ishara ya Kanisa, lililo bibi harusi wa Kristo, unalolitakatifuza kwa kazi isiyokoma. Nalo Kanisa, lililo mama anayewafurahia watoto wake wasiohesabika, lifikishwe mbinguni katika utukufu wako.
Kwa hiyo, sisi pamoja na umati mkuu wa watakatifu na malaika wote tunakutukuza, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Pet.2:5
Kama mawe yaliyo hai mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu, wewe umependa kutupatia ishara ya Yerusalemu ya mbinguni kwa njia ya Kanisa lako la hapa duniani. Tunakuomba ili, kwa kushiriki sakramenti hii, tufanywe hekalu la neema yako na tujaliwe kuingia katika makao ya utukufu wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.