Generic placeholder image

Novemba 22
MTAKATIFU SESILIA Bikira na Mfiadini
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ndiye mfalme wa mabikira: njooni, tumwabudu (aleluya).

Au:
Mabikira humfuata Mwana-Kondoo ko kote aendako; njooni, tumwabudu (aleluya).

Au:
Mabikira humfuata Mwana-Kondoo ko kote aendako; njooni, tumwabudu (aleluya).

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.) Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Roho wa heri wa Mungu
Kamshauri bikira
Azitumie silaha
'Tika vita vya maisha:
Pweke afanye safari,
Kuachana nao mwili,
Aende mbele ya Bwana,
Bila kifungo cho chote.

Bikira alitazama
Msalaba wa Kristo,
Na yeye akampamba
Awe bi-arusi wake;
Matunda ya Roho kazaa,
Matunda ndo ya milele,
Ambayo huthibitisha
Amana ya Mungu ya pendo.

Maishaye lionesha
Utawala wake Bwana
Alipoishi kipweke
Kwa ajili yake Bwana,
Kumngoja kimya-kimya
Pamoja nao fukara,
Bikira alo mnyofu,
Bikira asiye waa.

Utatu Mtakatifu,
Taji yao mabikira,
Wakuimbia masifu
Kwa wimbo usiokoma,
Wao wanashangilia
Haja yao umewapa,
Bwana Mungu wewe ndiwe
Nguvu yao wenye nguvu.

ANT. I: Nitamshuhudia Kristo; Kristo ndiye ninayemtafuta; natamani kuungana na Kristo (aleluya).

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nitamshuhudia Kristo; Kristo ndiye ninayemtafuta; natamani kuungana na Kristo (aleluya).

ANT. II: Mabikira, mtukuzeni Bwana; yeye aliyepanda hekima yake ndani yenu, sasa analivika tunda mlilozaa (aleluya).

WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Mabikira, mtukuzeni Bwana; yeye aliyepanda hekima yake ndani yenu, sasa analivika tunda mlilozaa (aleluya).

ANT. III: Watakatifu watafurahia utukufu; ushindi wao unang'aa kutoka katika miili yao (aleluya).

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Watakatifu watafurahia utukufu; ushindi wao unang'aa kutoka katika miili yao (aleluya).

SOMO: Wim.8:7
Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha; Kama mtu angetoa badala ya upendo Mali yote ya nyumbani mwake, Angedharauliwa kabisa.

KIITIKIZANO
K. Moyo wangu umesema juu yako: Nimeutafuta uwepo wako, Bwana. (W. Warudie)
K. Uso wako ndio nitakaoendelea kuutafuta.
W. Nimeutafuta uwepo wako, Bwana.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Moyo wangu...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Ilikuwa karibu kumekucha, Sesilia alipopaaza sauti: Askari wa Kristo, yatupilieni mbali matendo ya giza, vaeni silaha zenu, muwe askari wa mwanga!

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Ilikuwa karibu kumekucha, Sesilia alipopaaza sauti: Askari wa Kristo, yatupilieni mbali matendo ya giza, vaeni silaha zenu, muwe askari wa mwanga!

MAOMBI
Kwa furaha kubwa tumtukuze Kristo, Bwana arusi wa mabikira wote.
W. Yesu, taji ya mabikira, utusikie.

Bwana Yesu, mabikira watakatifu walikupenda wewe kama mume wao pekee;
- tusitengane nawe kamwe. (W.)

Ulimtawaza mama yako Maria, awe malkia wa mabikira wote;
- kwa sala zake, utujalie tuweze kukutumikia kwa maisha safi. (W.)

Mabikira watakatifu walikufuata wewe kwa mioyo isiyogawanyika;
- usituruhusu tukumbwe na matamu ya ulimwengu huu unaopita, na hivyo kutengwa mbali nawe. (W.)

Bwana Yesu, wewe ndiwe bwana arusi, ambaye mabikira wenye busara walikuwa tayari kukulaki;
- utujalie tuungojee ujio wako kwa hamu na matumaini (W.)

Mtakatifu Sesilia, anayetawala katika ufalme wako, atuombee;
- kwa sala zake, utujalie hekima na maisha yasiyo na hatia. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, kwa huruma yako usikilize sala zetu, tunazokutolea chini ya ulinzi wa Mtakatifu Sesilia. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.