Generic placeholder image

Novemba 22
MTAKATIFU SESILIA Bikira na Mfiadini
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana pokea utenzi,
Utenzi wa shukurani,
Shukurani kwa ajili
Ya watakatifu wote
Hao walojitahidi
Katika wewe kuishi,
Walokufuata kweli,
Kwa ibada na utii.

Wote hao, hao wote,
Uzimani mautini,
Wakikwangalia wewe,
Wewe Bwana wao kweli,
Makubwa walijifunza
Kwa Roho Mtakatifu:
Yaani kuvumilia,
Na kutenda matukufu.

Basi kwa sababu hiyo,
Twatukuza jina lako,
Pia kwa unyenyekevu,
Twaomba, tunakusihi
Tuweze kufuatia
Utakatifu wa hao,
Tuweze ishi na kufa
Katika wewe Mwenyezi.

ANT. I: Kwa ajili yako nitajitunza safi. Nitakuja nikulaki, ewe bwana arusi, nikiwa nimechukua taa itoayo mwanga mkali, aleluya.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kwa ajili yako nitajitunza safi. Nitakuja nikulaki, ewe bwana arusi, nikiwa nimechukua taa itoayo mwanga mkali, aleluya.

ANT. II: Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu, aleluya.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu, aleluya.

ANT. III: Matumaini yangu thabiti hayataondolewa; msingi wake ni Kristo, kama nyumba iliyojengwa juu ya mwamba, aleluya.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Matumaini yangu thabiti hayataondolewa; msingi wake ni Kristo, kama nyumba iliyojengwa juu ya mwamba, aleluya.

SOMO: 1Kor.7:32,34
Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana, jinsi atakavyompendeza Bwana. Mwanamke asiyeolewa, au bikira, hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana.

KIITIKIZANO
K. Mabikira waja mbele ya mfalme. Wanaimba kwa furaha. (W. Warudie)
K. Wanaingia hekaluni mwa mfalme.
W. Wanaimba kwa furaha.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mabikira...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Sesilia, yule bikira, daima aliichukua injili ya Kristo moyoni mwake: mchana au usiku, kamwe hakukoma kusali na kuongea na Mungu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Sesilia, yule bikira, daima aliichukua injili ya Kristo moyoni mwake: mchana au usiku, kamwe hakukoma kusali na kuongea na Mungu.

MAOMBI
Kristo Bwana aliwasifu wale wanaoishi bila kutumia ndoa, kwa ajili ya utawala wa mbinguni. Tutangaze upendo wake, na tuombe:
W. Yesu, mfalme wa mabikira, utusikie.

Kristo Bwana wetu, ulilihusianisha Kanisa na wewe mwenyewe kama mwali bikira ahusianavyo na mumewe;
- uliwezeshe Kanisa hilo kuwa safi, takatifu na bila hatia. (W.)

Kristo Yesu, mabikira watakatifu walikulaki taa zao zikiwa zinawaka vizuri;
- uudumishe hai mwali wa uaminifu katika mioyo ya wanawake watawa. (W.)

Bwana, daima umeliwezesha Kanisa lako kuwa na imani iliyo safi na sahihi;
- uwajalie Wakristo wote imani iliyo ya kweli na kamili. (W.)

Unaleta furaha katika maisha ya waamini wako, wanapoadhimisha sikukuu ya bikira wako Mtakatifu Sesilia;
- uwawezeshe pia kufurahia maombezi yake ya daima. (W.)

Umewakaribisha mabikira wako watakatifu katika tafrija ya arusi ya mbinguni;
- uwaalike marehemu wote kwenye sikukuu ya uzima wa milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, kwa huruma yako usikilize sala zetu, tunazokutolea chini ya ulinzi wa Mtakatifu Sesilia. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.