MT. ANDREA MTUME
MASOMO
SOMO: Rum.10:9-18
Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua
katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata
kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti
ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa
kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije
yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri
kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana
Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeazimia habari zetu? Basi Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia
huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea
duniani mwote, na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:1-4(K)4
1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)
SHANGILIO: Mt.4:18
Aleluya, aleluya!
Bwana asema, Nifuateni, nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.
Aleluya!
INJILI: Mt.4:18-22
Yesu alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro,
na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni,
nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele,
akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye, ambao walikuwamo chomboni
pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba
yao, wakamfuata.
MAOMBI
Mungu amewafanya mitume kuwa mashahidi na watangazaji wa kwanza wa ufufuko wa Mwanae Yesu Kristo. Tumwombe Mungu ili kazi
ya kitume tuliyopewa kwa Ubatizo izae matunda ya wokovu.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Askofu wetu F. na wote walioirithi kazi ya mitume wako wazidi kuwa mfano bora wa umoja na upendo katika imani moja,
Bwana mmoja na Ubatizo mmoja. Ee Bwana.
2. Kwa maombezi ya Mt. Andrea mtume uwaamshie roho ya upendo, haki na amani duniani, wote wenye mamlaka katika serikali,
vyama vya siasa na jumuiya mbalimbali. Ee Bwana.
3. Ili waamini wote wasikie sauti yako inayowaita kuishi kadiri ya wito uliowaitia na waimarishwe katika kumshuhudia Kristo
kwa maneno na matendo mema. Ee Bwana.
4. Kwa ajili ya jumuiya (parokia) yetu, ili kwa kuumega mkate pamoja, na kwa mfano wa maisha yetu ya kitume, tukutukuze Wewe
Mungu na kuwavutia kwako ndugu zetu waliojitenga na Kanisa lako. Ee Bwana.
5. Ili, kwa sala za mitume wako, ndugu zetu marehemu F. wapokelewe katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Hayo tunayaomba kwako, Ee Mungu Baba, kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.