Novemba 30
MTAKATIFU ANDREA MTUME
JUMAMOSI JUMA LA 34
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho.
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Nendeni, mkahubiri Habari Njema ya utawala: mlipata bure;
toeni bure (aleluya).
Adhuhuri
Ant.: Nipo nanyi sikuzote, hata mwisho wa nyakati (aleluya).
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu (aleluya).
Zab.119:81-88 XI Sala wakati wa kudhulumiwa
Niko hoi kwa kukungojea uniokoe;*
naweka tumaini langu katika neno lako.
Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi.*
Nauliza: “Utakuja lini kunifariji?”
Nimekunjamana kama kiriba katika moshi,*
hata hivyo sijasahau amri zako.
Nitasubiri mpaka lini?*
Utawaadhibu lini wenye kunidhulumu?
Wenye kiburi, wasiojali sheria yako,*
wamenichimbia mashimo kunitega.
Amri zako zote ni za kuaminika;/
watu waongo wananidhulumu,*
tafadhali unisaidie!
Karibu wangefaulu kuniangamiza,*
lakini mimi sijavunja amri zako.
Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu,*
nipate kuzingatia maagizo yako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.61 Kuomba ulinzi
Sala ya mwadilifu atamaniye mambo ya mbinguni (Mt. Hilari)
Usikie kilio changu, Ee Mungu;*
usikilize sala yangu.
Ninakulilia ugenini humu;*
nikiwa nimevunjika moyo.
Unipeleke kwenye mwamba wa usalama,/
maana wewe ndiwe kimbilio langu,*
kinga yangu imara dhidi ya adui.
Uniruhusu nikae hemani mwako milele*
nipate usalama chini ya mabawa yako.
Ee Mungu, umezipokea nadhiri zangu,*
umenijalia mema uliyowaahidia wakuchao.
Umjalie mfalme maisha marefu,*
miaka yake iwe ya vizazi vingi.
Atawale milele mbele yako, Ee Mungu;*
mapendo na uaminifu wako vimlinde.
Hapo nitakuimbia nyimbo za sifa,*
nikizitekeleza kila siku nadhiri zangu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.64 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Zaburi hii hasa yatualika kuyafikiria mateso ya Bwana (Mt. Augustino)
Usikie, Ee Mungu, usikilize lalamiko langu;*
unilinde maisha yangu na vitisho vya adui.
Unikinge na njama za waovu,*
na ghasia za watu wabaya.
Wananoa ndimi zao kama upanga,*
wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale.
Toka mafichoni wanamshambulia mtu mnyofu,*
wanamshambulia ghafula bila kuogopa.
Wanashirikiana katika nia yao mbaya;/
wanapatana mahali pa kuficha mitego yao.*
Wakifikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona!”
Hufanya njama zao na kusema:/
"Sasa tumekamilisha mpango.*
Nani atagundua hila zetu?”
Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu!/
Lakini Mungu atawapiga mishale,*
na kuwajeruhi ghafula.
Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao;*
kila atakayewaona atatikisa kichwa.
Hapo watu wote wataogopa;/
watatangaza aliyotenda Mungu,*
na kufikiri juu ya matendo yake.
Waadilifu watafurahia aliyotenda Mungu,/
watakimbilia usalama kwake.*
Watu wote wema wataona fahari.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Nendeni, mkahubiri Habari Njema ya utawala: mlipata bure;
toeni bure (aleluya).
Adhuhuri
Ant.: Nipo nanyi sikuzote, hata mwisho wa nyakati (aleluya).
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu (aleluya).
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 2Kor.5:19b-20
Mungu ametupatia ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye
Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, patanishweni
na Mungu.
K. Sauti yao imeenea duniani kote (aleluya).
W. Ujumbe wao umesikika kote ulimwenguni (aleluya.)
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Mate.5:12a,14
Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Idadi ya watu waliomwamini Bwana,
waume kwa wake, iliongezeka zaidi na zaidi.
K. Walifuata maagizo ya Mungu (aleluya).
W. Walishika amri zake (aleluya).
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Mate.5:41-42
Mitume wakatoka nje ya ule mkutano wa halmashauri, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu walistahili
kuaibishwa kwa sababu ya jina la Yesu. Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari
Njema ya Kristo.
K. Furahini na shangilieni, Bwana alisema (aleluya).
W. Kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni (aleluya).
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulimwita Mtakatifu Andrea mtume wako ahubiri habari njema, na aliongoze
Kanisa lako. Kwa unyenyekevu tunasali, ili daima atuombee mbele yako. Tunaomba hayo kwa njia
ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.