Desemba 3
MTAKATIFU FRANSIS KSAVER Padre
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo ni mchungaji mkuu, kiongozi wa kundi lake; njooni, tumwabudu (aleluya).
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI
Watakatifu ambao
Kwa ta'bu walisafiri
Kuieneza Injili
Ya neema yake Mungu,
Sasa ndo wametulia
Huko uwinguni juu
Pamoja na Kristo
Waliyemtumikia.
Wao walikaa macho
Kungoja uwaamuru
Waende kila mahali
Lako neno kuhubiri;
Kweli Bwana walikwenda,
Na kote kote kupita,
Hali wamejawa ari,
Ari isiyozimika.
Ile kazi walofanya
Ni yakini kazi yako,
Injili walohubiri
Ni habari njema yako,
Na nguvu waloonyesha
Si yao bali ni yako,
Ni yako mateso yao,
Kwa'jili ya wanadamu.
ANT. I: Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa juu mlimani,
hauwezi kufichika (aleluya).
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa juu mlimani,
hauwezi kufichika (aleluya).
ANT. II: Nuru yenu ni lazima iangaze mbele ya watu, ili, wakiona
matendo yenu mema, waweze kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni (aleluya).
WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
ANT. II: Nuru yenu ni lazima iangaze mbele ya watu, ili, wakiona
matendo yenu mema, waweze kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni (aleluya).
ANT. III: Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko
upanga wenye makali kuwili (aleluya).
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko
upanga wenye makali kuwili (aleluya).
SOMO: Ebr.13:7-9a
Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni ujumbe wa Mungu. Fikirieni juu ya mwenendo wao,
mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yule yule, jana, leo na milele. Msipeperushwe huku na huku
kwa mafundisho tofauti ya kigeni.
KIITIKIZANO
K. Niliwaweka walinzi katika minara yako, Yerusalemu. (W. Warudie)
K. Hawataacha kusimulia juu ya jina la Bwana, mchana na usiku.
W. Katika minara yako, Yerusalemu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Niliwaweka...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Anayesema, si ninyi, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu (aleluya).
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Anayesema, si ninyi, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani
yenu (aleluya).
MAOMBI
Kristo, mchungaji mwema, aliutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Na tumsifu kwa mioyo ya
shukrani, tunaposali:
W. Bwana, uyastawishe maisha ya watu wako.
Kristo Bwana wetu, waonesha upendo wako kwetu kwa njia ya wachungaji watakatifu;
- utuwezeshe kufaidi daima maongozi ambayo unayaonesha kwa njia yao. (W.)
Kwa njia ya watumishi wako watakatifu, wewe unakuwa kati yetu, ukizichunga roho zetu;
- usiache kamwe kutuongoza kwa mafundisho yao, na kwa misaada yao ya kutia moyo. (W.)
Kwa njia ya watakatifu wanaoliongoza taifa lako, unadhihirisha uwezo wako wa kuponya roho na mwili;
- uwe pamoja nasi daima, ili uyafanye upya maisha yetu, yawe matakatifu zaidi na zaidi. (W.)
Kwa mfano wa watakatifu, unawafunza waamini wako kufuata njia za hekima na upendo;
- kwa njia ya wachungaji wetu, utusaidie tuweze kukua hata kuufikia upeo wa ukamilifu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, ulijipatia watu wa mataifa mengi kutokana na mahubiri ya Mtakatifu Fransis Ksaver. Utupatie
ari ya kueneza imani kama Fransis Ksaver alivyokuwa nayo, na ulijalie Kanisa lako kufurahia kuona fadhili
na idadi ya watoto wake inaongezeka ulimwenguni kote. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.