Desemba 3
MTAKATIFU FRANSIS KSAVER Padre
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Hawa ni akina nani
Watokeza kama nyota,
Hawa wanaosimama
Mbele ya kiti cha Mungu?
Kila yule amevaa
Taji safi ya dhahabu;
Ni akina nani hawa,
Hii jamii tukufu?
Sikiliza! wanaimba:
Aleluya, aleluya!
Kwa sauti wamsifu
Mfalme wao wa mbingu.
Hawa ndio wale wale,
Wale waloshindania
Hadhi ya Mwokozi wao
Kwa muda mrefu sana,
Ndio walioshindana
Kwa nguvu mpaka mwisho,
Bila kufwata mkumbo
Wa watu watenda dhambi;
Hawa waloendeleza
Mapambano kwa ufundi,
Wameupata ushindi
Kwa njia: Mwana - Kondoo.
Hawa makasisi wenu
Kakaa macho kingoja,
Wakitolea utashi
Kwa Kristo wao Bwana,
Roho na miili yao
Ilikuwa imetengwa
Ili kumtumikia
Kristo usiku mchana:
Sasa wenye heri hao
Mbele ya uso wa Mungu,
Mahali patakatifu,
Wamesimama wang'ara.
ANT. I: Nimepata kuwa mhudumu wa injili, kutokana na neema nyingi
za Mungu (aleluya).
Zab.15 Rafiki ya Mungu
Ee Mungu, nani awezaye kukaa hemani mwako?*
Nani awezaye kukaa juu ya mlima wako mtakatifu?
Ni mtu anayeishi bila hatia,*
atendaye daima yaliyo sawa,
asemaye ukweli kutoka moyoni,*
na ambaye hasengenyi watu.
Ni mtu ambaye hamtendei ubaya mwenzake,*
wala hamfitini jirani yake.
Mtu huyo huwadharau wafisadi,/
lakini huwaheshimu wamchao Mungu.*
Hutimiza ahadi yake hata kama ikimtia hasara.
Hukopesha bila kutaka faida,/
wala hali rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia.*
Mtu mwenye sifa hizo, atakuwa imara milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Nimepata kuwa mhudumu wa injili, kutokana na neema nyingi
za Mungu (aleluya).
ANT. II: Huyu ndiye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye
Bwana alimfanya awe mkuu wa nyumba yake (aleluya).
Zab.112 Furaha ya mtu mwema
Heri mtu anayemcha Mungu,*
anayefurahia sana kutii amri zake.
Watoto wake watakuwa wenye enzi duniani;*
wazao wake watabarikiwa.
Jamaa yake itakuwa tajiri,*
naye atakuwa na fanaka daima.
Watu wema huangaziwa mwanga wa furaha,/
kama vile taa iangazayo gizani;*
naam, watu wenye huruma, wapole na waadilifu.
Heri mtu mkarimu, akopeshaye bila faida;*
aendeshaye shughuli zake kwa kutumia haki.
Mwadilifu hatashindwa kamwe,*
na atakumbukwa daima.
Akipata habari mbaya haogopi;*
moyo wake ni thabiti na humtumainia Mungu.
Hana wasiwasi, wala haogopi nyoka;*
ana hakika adui zake watashindwa.
Huwapa maskini kwa ukarimu;/
wema wake haubadiliki.*
Mtu wa namna hiyo atasifika daima.
Waovu huona hayo na kuudhika;/
husaga meno kwa chuki na kutoweka,*
mambo huenda kinyume cha matazamio yao.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Huyu ndiye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye
Bwana alimfanya awe mkuu wa nyumba yake (aleluya).
ANT. III: Kondoo walio wangu huisikiliza sauti yangu; patakuwa na
kundi moja na mchungaji mmoja tu (aleluya).
WIMBO: Ufu.15:3-4
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!
Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako?*
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Kondoo walio wangu huisikiliza sauti yangu; patakuwa na
kundi moja na mchungaji mmoja tu (aleluya).
SOMO: 1Pet.5:1-4
Wazee! Mimi niliye mzee, ninalo ombi moja kwenu wazee wenzangu. Mimi mwenyewe nilishuhudia
kwa macho yangu mateso ya Kristo, na natumaini kuushiriki ule utukufu utakaofunuliwa. Mimi
nawaombeni mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze, si kwa kulazimika, bali
kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo, si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu
wote. Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo
kundi. Na, wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, ninyi mtapokea taji ya utukufu usiofifia.
KIITIKIZANO
K. Huyu ni mtu ambaye anawapenda ndugu zake, na anawaombea watu. (W. Warudie)
K. Aliutoa uhai wake kwa ajili ya ndugu zake.
W. Na anawaombea watu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Huyu ni mtu...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Huyu ni mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye Bwana alimpa mamlaka juu ya watu wa nyumbani
mwake, ili awape chakula wakati ufaao (aleluya).
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Huyu ni mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye Bwana alimpa
mamlaka juu ya watu wa nyumbani mwake, ili awape chakula wakati ufaao (aleluya).
MAOMBI
Tumwombe Kristo, kuhani mkuu, ambaye aliteuliwa awe mshenga kati ya watu na Mungu.
W. Bwana, uwaokoe watu wako.
Bwana Yesu, zamani uliliongoza taifa lako kwa njia ya watu watakatifu na wenye hekima;
- uwawezeshe Wakristo kufurahia daima ishara hii ya upendo wako mkuu. (W.)
Uliwasamehe watu wako dhambi zao walipoombewa na wachungaji watakatifu,
- kwa maombezi yao yenye nguvu, uendelee kulitakasa Kanisa lako. (W.)
Walipokuwa pamoja na ndugu zao, uliwateua hao watakatifu wako, na ukawashushia Roho wako;
- uwajaze Roho wako Mtakatifu viongozi wote wa taifa lako. (W.)
Hakuna kilichoweza kuwatenganisha wachungaji watakatifu na upendo wako;
- usimpoteze hata mmoja kati ya hao uliowakomboa kwa mateso yako. (W.)
Kwa njia ya wachungaji wa Kanisa lako, unawapatia kondoo wako uzima wa milele, na hakuna anayeweza
kukuibia kondoo hao;
- uwaokoe waamini marehemu, ambao kwa ajili yao uliutoa uhai wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, ulijipatia watu wa mataifa mengi kutokana na mahubiri ya Mtakatifu Fransis Ksaver. Utupatie
ari ya kueneza imani kama Fransis Ksaver alivyokuwa nayo, na ulijalie Kanisa lako kufurahia kuona fadhili
na idadi ya watoto wake inaongezeka ulimwenguni kote. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.