Desemba 7
MTAKATIFU AMBROSI askofu
JUMAMOSI JUMA LA 1 LA MAJILIO
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Ee Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Baba, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nimewatuma
hao ulimwenguni (aleluya).
Adhuhuri
Ant.: Mtu anayewapokea ninyi, hunipokea mimi: yeyote anayenipokea
mimi, humpokea Yeye aliyenituma (aleluya).
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Sisi twafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni bustani ya Mungu,
ni jengo la Mungu (aleluya).
Zab.119:33-40 V Kuomba maarifa
Ee Mungu, unioneshe kanuni zako,*
nami nitazishika mpaka mwisho.
Unieleweshe sheria yako,*
niishike kwa moyo wangu wote.
Uniongoze nishike amri zako,*
maana humo napata furaha.
Unipe ari ya kufuata sheria zako,*
sio tamaa ya kupata utajiri.
Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi;*
unifadhili kama ulivyoahidi.
Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako;*
ahadi unayowapa wanaokuheshimu.
Uniokoe na lawama ninazoogopa;*
maana hukumu zako ni safi.
Natamani sana kuzitii amri zako;*
unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.34 Sifa kwa wema wa Mungu
Mmeonja na kuona kuwa Bwana ni mwenye fadhili (1Pet.2:3)
I
Nitamtukuza Mungu nyakati zote,*
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
Nitamwonea Mungu fahari,*
wanaodhulumiwa wasikie na wafurahi.
Mtukuzeni Mungu pamoja nami,*
sote pamoja tulisifu jina lake.
Nilimwomba Mungu, naye akanisikiliza,*
akaniondolea hofu zangu zote.
Mgeukieni Mungu, mpate kufurahi;*
hamtapata kamwe kusikitika.
Maskini alimlilia Mungu, naye akamsikiliza,*
na kumwokoa katika shida zake zote.
Malaika wa Mungu huwalinda wote wamchao,*
na kuwaokoa katika hatari.
Jioneeni wenyewe jinsi Mungu alivyo mwema.*
Heri wanaokimbilia usalama kwake.
Mcheni Mungu, enyi watakatifu wake;*
wenye kumcha hawakosi mahitaji yao.
Hata simba huona njaa kwa kutindikiwa;*
bali wanaomtii Mungu wana kila kitu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Njoni, enyi vijana, mkanisikilize,*
nami nitawafundisheni kumcha Mungu.
Je, wapenda kufurahia maisha;*
kuishi maisha marefu na ya fanaka?
Basi, acha kusema mabaya;*
achana na hila.
Jiepushe na uovu, utende mema;*
tafuta amani na kuizingatia.
Mungu huwaangalia waadilifu,*
na kusikiliza malalamiko yao;
lakini huwapinga watendao mabaya,*
awaondoa duniani, wasahauliwa kabisa.
Waadilifu wakimlilia Mungu, huwasikiliza,*
na kuwaokoa katika taabu zao zote.
Mungu yu karibu na waliovunjika moyo;*
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
Mateso ya mwadilifu ni mengi,*
lakini Mungu humwokoa katika yote.
Mungu humlinda mtu mwadilifu,*
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
Ubaya utawaangamiza watu waovu;*
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
Mungu atawaokoa watu wake, *
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Baba, kama wewe ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nimewatuma
hao ulimwenguni (aleluya).
Adhuhuri
Ant.: Mtu anayewapokea ninyi, hunipokea mimi: yeyote anayenipokea
mimi, humpokea Yeye aliyenituma (aleluya).
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Sisi twafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni bustani ya Mungu,
ni jengo la Mungu (aleluya).
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 1Tim.4:16
Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo, maana ukifanya
hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.
K. Bwana alimchagua mtumishi wake (aleluya).
W. Alimwita awe mchungaji wa Yakobo, urithi wake (aleluya).
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Tim.1:12
Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo, aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa
kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie.
K. Sitaona aibu kutangaza Habari Njema (aleluya).
W. Uwezo wa Mungu ndio unaowaokoa watu (aleluya).
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 1Tim.3:13
Wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu
juu ya imani yao katika Kristo Yesu.
K. Kama Bwana haijengi nyumba hiyo (aleluya).
W. Wale waijengao wafanya kazi bure (aleluya).
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulimfanya Mtakatifu Ambrosi awe mwalimu wa imani Katoliki, na kielelezo cha
ushujaa wa kitume. Uwachague katika Kanisa siku hizi watu walio tayari kufanya upendavyo wewe, ili
waliongoze taifa lako kwa busara na nguvu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.