Generic placeholder image

Desemba 8
BIKIRA MARIA KUKINGIWA DHAMBI YA ASILI
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Na tuadhimishe Kukingiwa Dhambi ya Asili Bikira Maria. Tumwabudu Mwanae, ambaye ni Kristo Bwana.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Nuru takatifu waangaza
Katika upeo wa dunia,
Ndiwe nyota ya matumaini
Kwa watu walioanguka,
Ndiwe Nuru katika dunia -
Dunia ya giza na vivuli,
Ndiwe pambazuko la wokovu,
Chimbuko la mpango wa Mungu.

Tokea milele na milele,
Wewe Mama, wewe peke yako,
Kati yetu sisi watu wote
Umechaguliwa kweli kweli;
Ndipo kwa yale mastahili
Ya huruma kubwa ya Mwanao,
Wewe mimba ukachukuliwa
Bila ile dhambi ya asili.

Ewe Mzazi wa Mkombozi-
Huyo mkomboa ulimwengu,
Sisi wewe tuliahidiwa
Tangu mwanzo wa zote nyakati;
Jee, ingewezekana vipi
Wewe mama mpendwa kabisa
Ushirikishwe ile hatia
Ya uasi ovyo wa Adamu?

Jua, hali kadhalika mwezi,
Na hata nyota zinakupamba,
Ewe Eva usiye na dhambi,
Uliye Ishara ya ushindi;
Ndiwe uliyemponda-ponda
Kwa miguu yako yule nyoka;
Maria, wewe ndiwe amana
Ile ya uzima wa kimungu.

Dunia hii iliyo chini
Na mbingu iliyo juu sana,
Husifia sana utukufu
Wa hali yako, Ee Maria;
Wewe sasa ulovishwa taji,
Na ulo katika utukufu,
Ulitungwa mimba kwa mamako
Bila ile dhambi ya asili.

Salamu, ewe mama mpenzi,
Wewe akupendaye sana Baba,
Uliyepata kuwa mzazi -
Mama ya Mwanae wa pekee,
Wewe Bi-arusi wa ajabu,
Mke wake Pendo wa milele,
Salamu, ewe mzuri sana,
Heko, ewe usiye na waa.

ANT. I: Tazameni, Mama safi ambaye hakupata doa, alichaguliwa awe Mama wa Mungu.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Tazameni, Mama safi ambaye hakupata doa, alichaguliwa awe Mama wa Mungu.

ANT. II: Umebarikiwa, Ee Bikira Maria, kuliko wanawake wote duniani. Bwana Mungu mwenyewe amekuchagua.

WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Umebarikiwa, Ee Bikira Maria, kuliko wanawake wote duniani. Bwana Mungu mwenyewe amekuchagua.

ANT. III: Yanukia vizuri harufu ya manukato yako, ewe Bikira usiye na waa. Na tuzifuate nyayo zako.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Yanukia vizuri harufu ya manukato yako, ewe Bikira usiye na waa. Na tuzifuate nyayo zako.

SOMO: Isa.43:1
Sasa, BWANA aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi: Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.

KIITIKIZANO
K. Bwana Mungu hunizungushia nguvu. (W. warudie)
K. Hunihifadhi nisipate doa la dhambi.
W. Hunizungushia nguvu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana Mungu akaliambia lile joka: Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake. Atakiponda kichwa chako, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana Mungu akaliambia lile joka: Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake. Atakiponda kichwa chako, aleluya.

MAOMBI
Tutangaze ukuu wa Mwokozi wetu, aliyechagua kuzaliwa na Bikira Maria. Tukitumaini kwamba atatusikiliza, tuombe:
W. Usikilize maombezi ya mama yako.

Jua la haki, siku yako ilipambazuka katika Bikira Maria asiye na doa;
- utusaidie tuenende katika mwanga wa uwepo wako. (W.)

Mwokozi wa ulimwengu, kwa nguvu yako ya kukomboa, ulimkinga mama yako na kila doa la dhambi;
- utuopoe kutoka katika uovu uliojificha mioyoni mwetu. (W.)

Kristo, Mkombozi wetu, ulimfanya Bikira Maria awe makao yako, na awe hekalu la Roho;
- utufanye tuwe makao ya Roho wako. (W.)

Mfalme wa wafalme, ulimpaliza Maria mbinguni, ili awe pamoja nawe, mwili na roho;
- utuwezeshe kuyatafuta yaliyo ya juu, na kuyaelekeza maisha yetu kwako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba, tunafurahi upendeleo uliomfanyia Bikira Maria hata akazaliwa bila dhambi, upendeleo ambao ulimkinga na doa la dhambi kwa nguvu ya kifo cha Kristo kiletacho ukombozi, na ambao ulimtayarisha awe Mama wa Mungu. Utujalie, kwa maombezi yake, sisi wenyewe tufike kwako, hali tumetakaswa na kila dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.