SIKUKUU YA
BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI
8 DESEMBA
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.61:10
Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu, maana amenivika mavazi ya
wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.
UTUKUFU Husemwa
KOLEKTA
Ee Mungu, ulimwandalia Mwanao makao stahiki, kwa kutungwa mimba Bikira Maria bila doa la dhambi. Tunakuomba
ili, kama ulivyomkinga dhidi ya doa lolote la dhambi kwa ajili ya kifo cha Mwanao kilichotazamiwa, nasi pia
utujalie, kwa maombezi ya Bikira Maria, tuwe safi hadi kufika kwako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mwa.3:9-15,20
Adamu baada ya kula matunda ya mti, Bwana Mungu akamwita, akamwambia, Uko wapi? akasema, Nalisikia sauti
yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, ni nani aliyekuambia ya kuwa u
uchi? Je, umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyu mwanamke uliyenipa awe
pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili
ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu
umeyafanya hayo, umelaaniwa Wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo
utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke,
na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa. na wewe utamponda kisigino. Adamu akamwita mkewe
jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4 (K)1
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
2. Bwana ameufunua wokovu wake.
machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. (K)
3. Amezikumbuka rehema zake,
na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
Miisho yote ya dunia imeuona
wokovu wa Mungu wetu. (K)
4. Mshangilieni Bwana, nchi yote,
inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
SOMO 2: Efe.1:3-6,11-12
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu
wa roho, ndani yake Kristo. Kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu,
ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili
tufanywe wanawe kwa njia ja Yesu Kristo, sawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake,
ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa
tangu awali sawa sawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi
katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
SHANGILIO: Lk.1:28
Aleluya, aleluya!
Salamu, Mariamu, umejaa neema, Bwana yu pamoja nawe,
umebarikiwa kuliko wanawake wote.
Aleluya!
SOMO 3: INJILI: Lk.1:26-38
Siku ile malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali
bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi, na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
Akaingia nyumbani mwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa
ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu,
kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita
Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, Baba
yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia
malaika, Litakuwaje neno hili, maana simjui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia
juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli, kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa
kitakatifu, Mwana Wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elizabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume
katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana
kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika
akaondoka akaenda zake.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Kwa Ubatizo, kila Mwanadamu anaondolewa dhambi ya asili. Lakini tunahitaji bado neema za Mungu ili
tusiendelee kutenda dhambi. Basi, Ee Mungu, kwa maombezi ya Bikira Maria Imakulata, twakuomba:
1. Uwaimarishe viongozi wote wa Kanisa katika kushikilia nguzo zote za imani ya Kanisa lako bila
kutetereka.
2. Viongozi wa serikali zote duniani waungane na raia wao kupambana na maovu yanayolaaniwa siku zote.
3. Kwa kuwa ulitangulia kutuchagua ili tufanywe wanao kwa njia ya Yesu Kristo, utufanye watakatifu na bila
hitilafu mbele yako.
4. Sisi sote tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu, utujalie neema yako ili tusianguke katika kiburi cha
wazazi wetu wa kwanza.
5. Maria Mama wa Yesu alisema: “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena.” Utujalie maishani
mwetu unyenyekevu kama wa Maria.
6. Wana wa Adamu wote wanaozaliwa waondolewe dhambi ya asili, ili wabaki bila doa; na marehemu
wetu F. watakaswe dhambi zao na kulakiwa huko mbinguni na Mama yako Mkingiwa
dhambi ya asili.
Ee Mungu, Mama yako ni Mama yetu. Utujalie kumpenda na kumheshimu siku zote na, kwa maombezi yake, wabatizwa
wote tupewe msamaha wa dhambi na mastahili ya kufika huko aliko. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakutolea sadaka iletayo wokovu katika sherehe ya kutungwa mimba bila doa Bikira Maria mtakatifu.
Uwe radhi kuipokea, na utujalie ili, kama vile tunavyoungama kuwa yeye alikingiwa kila doa la dhambi kwa
neema yako tangulizi, nasi pia, kwa maombezi yake, tuwekwe huru na kila dhambi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI: Fumbo la Maria na Kanisa.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba
uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe ulimkinga Bikira Maria mtakatifu sana na doa lolote la dhambi ya asili, ili akitajirishwa na utimilifu
wa neema yako, uweze kumtayarishia Mwanao mama stahiki, na kudokeza katika yeye mwanzo wa Kanisa lililo Bibi
harusi wake mtukufu, lisilo na ila wala kunyanzi.
Bikira mwenye usafi kamili alituzalia Mwana, ambaye, kama Mwanakondoo asiye na waa, anaondoa hatia zetu.
Nawe umemwinua Maria kuliko wote, kwa ajili ya watu wako, kusudi awe mwombezi wa neema na mfano wa utakatifu.
Kwa hiyo, pamoja na Malaika wa mbinguni, tunakusifu tukiungama kwa furaha:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi...
ANTIFONA YA KOMUNYO:
Matukufu yamenenwa juu yako Maria, kwa sababu kutoka kwako limechomoza jua la haki, Kristo Mungu wetu.
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu wetu, tunakuomba sakramenti tuliyopokea iponye ndani yetu madonda ya dhambi ile ambayo ulimkinga
kwa namna ya pekee Maria mwenye heri kwa kutungwa mimba bila doa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.