Generic placeholder image

Desemba 8
BIKIRA MARIA KUKINGIWA DHAMBI YA ASILI
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI tazama pia AU
Nuru takatifu waangaza
Katika upeo wa dunia,
Ndiwe nyota ya matumaini
Kwa watu walioanguka,
Ndiwe Nuru katika dunia -
Dunia ya giza na vivuli,
Ndiwe pambazuko la wokovu,
Chimbuko la mpango wa Mungu.

Tokea milele na milele,
Wewe Mama, wewe peke yako,
Kati yetu sisi watu wote
Umechaguliwa kweli kweli;
Ndipo kwa yale mastahili
Ya huruma kubwa ya Mwanao,
Wewe mimba ukachukuliwa
Bila ile dhambi ya asili.

Ewe Mzazi wa Mkombozi-
Huyo mkomboa ulimwengu,
Sisi wewe tuliahidiwa
Tangu mwanzo wa zote nyakati;
Jee, ingewezekana vipi
Wewe mama mpendwa kabisa
Ushirikishwe ile hatia
Ya uasi ovyo wa Adamu?

Jua, hali kadhalika mwezi,
Na hata nyota zinakupamba,
Ewe Eva usiye na dhambi,
Uliye Ishara ya ushindi;
Ndiwe uliyemponda-ponda
Kwa miguu yako yule nyoka;
Maria, wewe ndiwe amana
Ile ya uzima wa kimungu.

Dunia hii iliyo chini
Na mbingu iliyo juu sana,
Husifia sana utukufu
Wa hali yako, Ee Maria;
Wewe sasa ulovishwa taji,
Na ulo katika utukufu,
Ulitungwa mimba kwa mamako
Bila ile dhambi ya asili.

Salamu, ewe mama mpenzi,
Wewe akupendaye sana Baba,
Uliyepata kuwa mzazi -
Mama ya Mwanae wa pekee,
Wewe Bi-arusi wa ajabu,
Mke wake Pendo wa milele,
Salamu, ewe mzuri sana,
Heko, ewe usiye na waa.

AU
Bikira, na papo hapo ni Mama,
Binti yake Mwana wako mwenyewe,
U juu kuliko wengine wote -
Ila hapana wa chini zaidi;
Wewe ndio utimilifu wote
Ulopangwa kwa amri ya Mungu
Ulimwengu wetu uloanguka
Katika wewe lipokuwa bora!

Akisha tayarishiwa mahali,
Yeye aliyeumba vitu vyote
Kakaa kati ya viumbe vyake,
Kifuani pako ndo akalala;
Hapo akalisha upendo wake-
Kwa joto ambalo liliukuza
Mzizi ule ulostawisha
Amani yetu sisi ya milele.

Na si peke yako usikiaye
Sisi tunaposifu lako jina;
Mara nyingi huwa karibu sana
Sauti zetu zinapokatika;
Viumbe vyote kaumbwa vizuri
Kwa umbo na kwa sura yako nzuri,
Huruma, nguvu, upole na wema,
Na neema umejaliwa mama.

Bibi, tushindwapo kuona mbele,
Katika kutarajia ya mbingu,
Endelea bado kutuombea
Sisi kwa huyo Mwanao daima,
Ambaye anastahili sifa,
Nguvu na enzi na wote uweza,
Pamoja na Roho Mtakatifu,
Na pamoja na Baba mtukufu.

ANT. I: U mzuri kabisa, Ee Maria; huna dhambi ya asili.

Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“

Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!

Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!

Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.

Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.

Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!

Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“

Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!

Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: U mzuri kabisa, Ee Maria; huna dhambi ya asili.

ANT. II: Wewe ni utukufu wa Yerusalemu, wewe ni furaha ya Israeli! Wewe ni heshima kuu kabisa ya kabila letu.

Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.

Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.

Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?

Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!

Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.

Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.

Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wewe ni utukufu wa Yerusalemu, wewe ni furaha ya Israeli! Wewe ni heshima kuu kabisa ya kabila letu.

ANT. III: Mavazi yako ni meupe kama theluji, uso wako unang'aa kama jua.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mavazi yako ni meupe kama theluji, uso wako unang'aa kama jua.

SOMO: Rom.5:20-21
Pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi. Kama vile utawala wa dhambi uletavyo kifo, utawala wa neema huleta uadilifu, na mwishowe, uzima wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

KIITIKIZANO
K. Kwa hilo nitajua kwamba umenichagua. (W. warudie)
K. Kama adui yangu hatanishinda.
W. Nitajua kwamba umenichagua.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kwa hilo...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Salaam, Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Salaam, Maria, umejaa neema: Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa, aleluya.

MAOMBI
Tumtukuze Mungu Baba, aliyemchagua Maria awe mama ya Mwanae, na aliyetaka vizazi vyote vimwite ni mwenye heri. Kwa imani na matumaini tuombe:
W. Maria Mtakatifu, utuombee.

Baba, ulifanya mambo makuu kwa ajili ya Bikira Maria, na ukamfikisha, mwili na roho, kwenye utukufu wa mbinguni;
- ujaze mioyo ya watoto wako matumaini ya kupata utukufu wa Kristo. (W.)

Kwa maombezi ya Maria, mama yetu, uwaponye wagonjwa, uwatulize wenye huzuni, uwasamehe wenye dhambi;
- uwajalie watu wote amani na wokovu. (W.)

Ulimjalia Maria neema tele;
- uwashushie watu wote baraka zako kwa wingi. (W.)

Uliunganishe Kanisa lako, liwe moyo mmoja na roho moja, kwa nguvu ya upendo;
- na uwawezeshe waanini wako kujiunga na Maria, mama ya Yesu, katika kusali daima. (W.)

Baba, umemtukuza Bikira Maria, na kumfanya awe malkia wa mbingu;
- uwajalie marehemu kuingia katika ufalme wako, na kufurahi pamoja na watakatifu wako milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba, twafurahia upendeleo uliomfanyia Bikira Maria hata akazaliwa bila dhambi, upendeleo ambao ulimkinga na doa la dhambi kwa nguvu ya kifo cha Kristo kiletacho ukombozi, na ambao ulimtayarisha awe Mama wa Mungu. Utujalie, kwa maombezi yake, sisi wenyewe tufike kwako, hali tumetakaswa na kila dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.