Desemba 8
BIKIRA MARIA KUKINGIWA DHAMBI YA ASILI
SALA ZA MCHANA
chagua SALA YA ADHUHURI
chagua SALA BAADA YA ADHUHURI
Kwa SALA KABLA YA ADHUHURI: endelea hapo chini
KABLA YA ADHUHURI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;.
Na yote yanafanyika.
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu.
Milele inayodumu.
ANT.: Msifuni Mungu, ambaye hajaiondoa kwangu huruma yake.
Zab.120 Kuomba msaada
Muwe na saburi katika shida; salini daima (Rom.12:12)
Nilipokuwa katika taabu,*
nilimwita Mungu, naye akanisikiliza.
Ee Mungu, uniokoe*
na watu wadanganyifu na waongo.
Enyi watu wadanganyifu,*
mtapewa kitu gani?
Mtafanyiwa kitu gani zaidi?*
Mtaadhibiwa namna gani?
Kwa mishale mikali ya askari,*
kwa makaa ya moto!
Kukaa kati yenu ni balaa kama kukaa Mesheki*
au kama kukaa kati ya watu wa Kedari.
Nimeishi muda mrefu mno*
kati ya watu wanaochukia amani!
Mimi nataka' amani;/
lakini nisemapo juu ya amani,*
wao hutaka vita.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.121 Mungu kinga yetu
Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena (Ufu.7:16)
Ninatazama huko juu milimani;*
msaada wangu watoka wapi?
Msaada wangu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.
Hatakuacha uanguke;*
mlinzi wako hasinzii.
Mlinzi wa Israeli*
hasinzii wala halali.
Mungu anakulinda na kukukinga;*
yuko pamoja nawe kukulinda.
Mchana jua halitakuumiza,*
wala mwezi wakati wa usiku.
Mungu anakukinga na majanga yote;*
anayalinda salama maisha yako.
Anakulinda ujapo na uendapo,*
sasa na hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Ninyi mmefika mlimani Sion, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa
mbinguni (Ebr.12:22)
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu“
Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!
Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!
Humo ndimo makabila yanafika,/
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.
Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.
Uombeeni Yerusalemu amani;*
"Wote wakupendao wafanikiwe!
Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuwemo usalama!"
Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
ee Yerusalemu, nakutakia amani!
Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant.: Msifuni Mungu, ambaye hajaiondoa kwangu huruma yake.
SOMO: Ef.1:4
Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo, ili tuwe
watakatifu, na bila hitilafu mbele yake.
K. Leo tunaadhimisha Kukingiwa Dhambi ya Asili Bikira Maria Mwenye Heri.
W. Ambaye alikiponda-ponda kichwa cha lile joka kwa mguu wake.
SALA:
Tuombe: Baba, tunafurahi upendeleo uliomfanyia Bikira Maria hata akazaliwa bila dhambi, upendeleo
ambao ulimkinga na doa la dhambi kwa nguvu ya kifo cha Kristo kiletacho ukombozi, na ambao
ulimtayarisha awe Mama wa Mungu. Utujalie, kwa maombezi yake, sisi wenyewe tufike kwako, hali
tumetakaswa na kila dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.