Des 27 Mt. Yohane Mwinjili
MASOMO
SOMO 1: 1Yoh.1:1–4
Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono
yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima; na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia,
na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu; hilo tuliloliona na
kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na
Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.97:1–2,5–6,11–12
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake. (K)
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.
2. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake. (K)
3. Nuru imemzukia mwenye haki,
Na furaha wanyofu wa moyo.
Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana,
Na kulishukuru jina lake takatifu. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.
INJILI: Yn.20:2–8
Siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena alikwenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi
mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi
Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili;
na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini. Akainama
na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata,
akaingiza ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala
pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi
mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini.
MAOMBI
Ndugu, Mt. Yohane Mtume na Mwinjili ni mfano bora wa usafi wa Moyo na mapendo yasiyogawanyika. Tumwombe Mungu,
ili kwa maombezi yake furaha yetu itimizwe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie wote wenye maisha ya wakfu fadhila ya uaminifu, ili daima wawe mfano mwema wa usafi wao wa moyo.
2. Uwakirimie mapendo ya kidugu walezi wote wa vijana, waseminari na watawa ili, kwa neema yako, wapate roho
ya kitume isiyo na doa lolote.
3. Utusaidie sisi sote kuwa mashahidi wa Injili yako na tuwe wepesi wa kuitikia sauti yako, kama alivyofanya
Mt. Yohane Mtume na Mwinjili.
4. Uwaondolee marehemu wetu wote vikwazo vinavyowazuia kushirikishwa ufufuko wa Mwanao.
Ee Bwana, twakiri kuwa ushirika wetu ni pamoja nawe Baba, na pamoja na Mwana wako Yesu Kristo. Utujalie
bidii ya kukutafuta na kukutangaza wewe kwa maneno na matendo kama alivyofanya Mt. Yohane Mtume na
Mwinjili. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.