WATOTO MASHAHIDI
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Tumwabudu Kristo mchanga; leo aliwapatia Watoto watakatifu taji ya wafiadini.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI
Wafiadini waishi
Pamoja na Kristo,
Kale walijaribiwa
Kwa maumivu makali,
Upendo wao mkubwa
Uchungu uliondoa
Hao walipotundikwa
Na kufa msalabani.
Karne hata karne
Twapata wafiadini,
Waja kwa mtiririko
Bila ya mabadiliko.
Mioyo mejaa pendo
Wala hawalalamiki,
Walidhihirisha pendo
Kimya bila ya vituko.
Hapana mtu ye yote
Aloupima upendo,
Au kwa yake mikono
Kukadiria uzito,
Bali Mungu ajuaye
Yalo moyoni mwa mtu
Ndiye anawapatia
Ile nchi ya ahadi.
Tukuzwe Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Nyie mnatuongoza
Salama katika giza
Tukizifuata njia
Zinazozipita nyota
Na kufika kwenye nuru,
Kwenye nuru ya milele.
ANT. I: Watatembea pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, asema
Bwana, kwa sababu wanastahili.
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Watatembea pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, asema
Bwana, kwa sababu wanastahili.
ANT. II: Watoto wanamwimbia Mungu sifa; katika kifo wanahubiri kile
ambacho vinywa vyao vichanga havikuweza kutamka.
WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Ant. II: Watoto wanamwimbia Mungu sifa; katika kifo wanahubiri kile
ambacho vinywa vyao vichanga havikuweza kutamka.
ANT. III: Midomo ya watoto, wakubwa kwa wachanga, imekusifu na kumwaibisha adui yako.
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Midomo ya watoto, wakubwa kwa wachanga, imekusifu na kumwaibisha adui yako.
SOMO: Yer.31:15
BWANA asema hivi: Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto
wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako.
KIITIKIZANO
K. Hawa walikuwa watakatifu wa Mungu. Wataishi milele. (W. Warudie)
K. Bwana mwenyewe ni tuzo lao.
W. Wataishi milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Hawa...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Watoto hao wasio na hatia, waliuawa badala ya Kristo; watoto wachanga hao waliuawa na mfalme
mwovu: wanamfuata Mwana-Kondoo asiye na dhambi, wanaimba sifa zake, wakisema: Utukufu kwako,
Ee Bwana.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Watoto hao wasio na hatia, waliuawa badala ya Kristo; watoto
wachanga hao waliuawa na mfalme mwovu: wanamfuata Mwana-Kondoo asiye na dhambi, wanaimba sifa
zake, wakisema: Utukufu kwako, Ee Bwana.
MAOMBI
Bwana Yesu, hata ulipozaliwa, wanadamu walikuchukia, na watoto walikuwa ndio wa kwanza kuteseka
kwa ajili yako. Tunatangaza jinsi tunavyokutumainia:
W. Bwana yu ubavuni pangu: sitaogopa.
Kama wewe ulivyodhulumiwa, ndivyo na ndugu zako watakavyodhulumiwa.
- Bwana Yesu, tunatazamia msaada wako. (W.)
Hukutenda dhambi: hata hivyo, kama sisi, ilikupasa kuteseka.
- Utusaidie tuweze kuuchukua msalaba wetu, na kukufuata wewe. (W.)
Watoto hao Watakatifu walikushuhudia kimyakimya,
- utujalie tukutangaze kwa wengine kwa maneno na matendo. (W.)
Ulipokuwa mtoto ulidhulumiwa, ukafukuziwa uhamishoni:
- uwaokoe watoto wote wa wanadamu ambao wapo uhamishoni, au katika mateso makali. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, watoto wale Watakatifu walikushuhudia, si kwa kusema, bali kwa kufa: ujalie imani
tunayoitangaza kwa maneno, idhihirishwe kwa matendo. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima
na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.