Des 28 Watoto Wat. Mashahidi
MASOMO
SOMO 1: 1Yoh.1:5:2:2
Hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lolote
hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala
hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru twashirikiana sisi kwa
sisi, na damu yake Yesu Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya
wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee
dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo
wala neno lake halimo mwetu. Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu
akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu;
wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.124:1-4,7-8
1. Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia. (K)
(K) Nafsi yetu imeokoka kama ndege, katika mtego wa wawindaji.
2. Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu;
Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu. (K)
3. Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
Msaada wetu u katika jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.
INJILI: Mt.2:13-18
Mamajusi walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka,
umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta
mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa
Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.
Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto
wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa
muda ule aliohakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti
ilisikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.
MAOMBI
Leo tunakumbuka jinsi watoto wadogo walivyozimwaga damu zao kwa ajili ya kushiriki mateso ya Kristo.
Tumwombe Mungu, ili nasi tuwe mashahidi wa kweli wa Injili yake.
1. Wote wenye mamlaka na wajibu wa kulihubiri neno lako wajibidishe kukutangaza wewe Mungu, kuwa ni
nuru isiyo na giza lolote ndani yake.
2. Viongozi wote wa dini, serikali na vyama yote vya siasa wasiwaonee wivu wala kuwatenda vibaya wale
wote wanaokuja nyuma yao na vipawa vya uongozi bora; bali wawapokee kwa furaha na ushirikiano mwema.
3. Wafuasi wote wa Mwanao washirikiane nawe kulifukuza giza la dhambi, ili waishi maisha ya mwanga
yenye haki, amani, usawa na upendo wa kweli.
4. Utujalie sisi sote kuwajali watoto wetu na kuvikuza vipaji vyao ili, wakishapata malezi bora tangu
tumboni mwa mama zao, waweze kuwa mashahidi waaminifu wa Injili yako.
Ee Mungu uliyemwita Mwanao kutoka Misri, ulikubali damu ya Watoto wako Mashahidi imwagike ingawa
hawakuwa na hatia yoyote, ili kutufundisha ukubwa wa gharama ya wokovu wetu uliokamilishwa na Mwanao
pale msalabani. Utupe nasi moyo wa kujitoa sadaka kama mashahidi na watoto wako watakatifu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.