DES. 30 OKTAVA YA NOEL
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina, Aleluya.
UTENZI
Kristo, uliyemwaga damu yako
Kwa ajili ya wanadamu wote,
Ewe Mwangaza uliyeangaza
Kabla jua halijachomoza,
Mungu na Mwanae Mungu milele,
Mungu mmoja na Baba milele.
Wewe ndiwe utukufu halisi,
Utukufu wa nuru yake Baba;
Wewe u nyota ya matumaini,
Nyota ile ing'arayo daima;
Sikiliza za watu wako sala
Zitokazo huku kwetu bondeni.
Bwana, kumbuka hukulazimishwa,
Bali ni kwa pendo lako mwenyewe,
Kiticho cha enzi ulikiacha
Mbinguni ulikiacha mwenyewe,
Ubinadamu duni ukatwaa
Kwa kuzaliwa na Bikira safi.
Na kwa hiyo basi Kanisa lako,
Kila mwaka ujao na wendao,
Huadhimisha lile pendo lako,
Ambalo huvutia zetu nyoyo,
Pendo lilokushusha duniani
Uondoe za wakosefu dhambi.
Si dunia peke yake, hapana,
Yenye wajibu wa kushangilia,
Bali bahari nazo mbingu pia,
Ziimbe kwa sauti wimbo mpya,
Siku ya leo kuishangilia
Alozaliwa Bwana wa uzima.
Na usifiwe, Ee Yesu Bwana,
Ewe Mwana wa Bikira Maria,
Sifa hizo na zikujie sasa
Na hata milele zikufikie;
Na pia utukuzwe, Ewe Baba,
Nawe Roho usifiwe milele.
ANT. I: Mamlaka na utawala wote ni mali yako siku ya uwezo wako;
unang'ara kwa utakatifu. Kabla ya alfajiri nilikuzaa.
Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,
Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."
Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"
Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.
Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.
Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.
Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Mamlaka na utawala wote ni mali yako siku ya uwezo wako;
unang'ara kwa utakatifu. Kabla ya alfajiri nilikuzaa.
ANT. II: Bwana anao upendo usio na mipaka. Uwezo wake wa kuokoa watu ni mkuu.
Zab.130 Kuomba msaada
Katika unyonge wangu, nakulilia, Ee Mungu./
Ee Bwana, sikiliza sauti yangu,*
uitegee sikio sauti ya ombi langu.
Kama, Ee Mungu, ungeweka kumbukumbu ya madhambi yetu,*
ni nani, Ee Bwana, angeweza kusimama mbele yako?
Lakini wewe watusamehe dhambi,*
ili tukutumikie kwa uchaji.
Naweka tumaini langu lote kwa Mungu;*
nina imani sana na neno lake.
Namngojea Mungu kwa hamu kubwa,/
kuliko mlinzi usiku anavyongojea pambazuko;*
kuliko walinzi wanavyongojea kupambazuke.
Ee Israeli, umtumainie Mungu,/
maana yeye ni mwenye upendo mkuu;*
daima yuko tayari kutuokoa.
Naam, atawaokoa watu wa Israeli,*
katika maovu yao yote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana anao upendo usio na mipaka. Uwezo wake wa kuokoa watu ni mkuu.
ANT. III: Mwanzoni na kabla ya nyakati zote, Neno alikuwa Mungu; leo amezaliwa
kwetu, Mwokozi wa dunia.
WIMBO: Kol.1:12-20
Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu
katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.
Yeye alituokoa katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,
ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.
Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,
vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.
Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.
Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.
Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,
ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.
Maana Mungu mwenyewe aliamua/
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.
Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.
Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,
na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Mwanzoni na kabla ya nyakati zote, alikuwa Mungu; leo
amezaliwa kwetu, Mwokozi wa dunia.
SOMO: 2Pet.1:3-4
Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha
Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo
ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa
tamaa mbaya zilizoko duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu.
KIITIKIZANO
K. Neno akatwaa mwili, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Na akakaa kwetu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Neno akatwaa...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tunakutukuza, Mama wa Mungu; kwa kuwa ulimzaa Kristo. Uwakinge na maovu wale wote wanaokuheshimu.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Tunakutukuza, Mama wa Mungu; kwa kuwa ulimzaa Kristo. Uwakinge na maovu wale wote
wanaokuheshimu.
MAOMBI
Tumtangaze Kristo kwa furaha, kwa kuwa kutoka Betlehemu, katika nchi ya Yuda, amepatikana kiongozi
anayeliongoza taifa lake takatifu.
W. Bwana, neema yako iwe nasi.
Kristo, Mwokozi wetu, ongea nao wote ambao hawajasikia jina lako;
- uwavutie watu wote kwako. (W.)
Bwana, uyaingize mataifa yote katika Kanisa lako,
- ili wanadamu wote wapate kuwa taifa la Mungu. (W.)
Mfalme wa wafalme, ongoza akili na mioyo ya watawala;
- uwasaidie watafute amani kwa njia za haki. (W.)
Uwajalie imani wale wanaoishi katika mashaka,
- na uwape tumaini wale wanaoishi kwa hofu. (W.)
Uwafariji walio na huzuni, na uwatulize wale walio mahututi;
- uwaburudishe kwa wingi wa neema zako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Baba Mwenyezi, kuzaliwa kwa Mwanao wa Pekee kulikuwa ndio mwanzo wa maisha mapya.
Tunaomba atuopoe kutoka katika utumwa wa dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.