DES. 30 OKTAVA YA NOEL
SALA YA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama ya Yesu, walistaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.
Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu ulioandaa machoni pa watu wote.
Zab.19B:7-14. Sheria ya Mungu
Basi, mwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu (Mt.5:48)
Sheria ya Mungu ni kamilifu,*
humrudishia mtu nguvu;
agizo la Mungu ni thabiti,*
huwapa hekima wasio na makuu.
Amri za Mungu ni sawa,*
hufurahisha moyo;
agizo la Mungu ni la haki,*
humwelimisha mtu.
Kumcha Mungu ni jambo jema,*
uchaji wa Mungu wadumu milele;
hukumu za Mungu ni sawa,*
zote nizahaki kabisa.
Zatamanika kuliko dhahabu;*
kulikodhahabu safi kabisa.
Ni tamu kuliko asali;*
kuliko asali safi kabisa.
Zanifunza mimi mtumishi wako;*
kuzitii kwaniletea tuzo kubwa.
Lakini nani ayaonaye makosa yake mwenyewe?*
Ee Mungu, niepushe na makosa yale nisiyoyajua.
Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi,*
usikubali hayo yanitawale.
Hapo nitakuwa mkamilifu;*
sitakuwa na dhambi kubwa.
Maneno na mawazo yangu yakupendeze, Ee Mungu,*
mwamba wa usalama wangu na mkombozi wangu!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.7 Sala ya mtu anayedhulumiwa
Hakimu yu karibu, tayari kuingia (Yak.5:9)
I
Ee Mwenyezi, Mungu wangu, nakukimbilia wewe;*
uniokoe na wote wanaonidhulumu, unisalimishe.
La sivyo, watakuja kama simba kunirarua,/
na mbali kunivutia,*
pasiwe na mtu wa kuniokoa.
Ee Mwenyezi, Mungu wangu!/
Kama nimetenda moja ya mambo haya:*
kama nimechafua mikono yangu kwa ubaya,
kama nimemtenda vibaya rafiki yangu,*
au nimemshambulia bila sababu adui yangu,
basi, adui na anifuatie na kunikamata;/
ayakanyage maisha yangu;*
nakuniulia mbali.
Ee Mungu, uje kwa ghadhabu yako;*
uikabili hasira ya adui zangu.
Inuka, Ee Mwenyezi,*
Wewe wataka daima haki itekelezwe.
Uyakusanye mataifa kando kando yako,*
nawe uwatawale kutoka juu.
Wewe, Ee Mungu, wayahukumu mataifa;/
unihukumu kwa kadiri ya uadilifu wangu,*
kadiri ya huo unyofu wangu.
Uukomeshe uovu wa watu wabaya,*
umwimarishe mtu mwema;
Ee Mungu utendaye haki,*
upimaye mioyo na akili.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Mungu ni ngao yangu inayonilinda;*
yeye awaokoa watu wanyofu.
Mungu ni hakimu wa haki;*
kila siku humwadhibu adui mwovu.
Watu wasipoongoka, Mungu atanoa upanga wake;*
atavuta upinde wake na kulenga shabaha.
Atatayarisha silaha zake za hatari,*
na kuipasha moto mishale yake.
Lakini waovu wamejaa udhalimu;*
wameshiba uovu na watazaa udanganyifu.
Wamewachimbia wengine mashimo,*
lakini wao wenyewe watatumbukia humo.
Ubaya wao utawarudia wao wenyewe;*
ukatili wao utawaangukia wao wenyewe.
Nami nitamsifu Mungu kwa sababu ya wema wake;*
nitaimba sifa zake Mungu, Mungu Mkuu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama ya Yesu, walistaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.
Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu ulioandaa machoni pa watu wote.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Kum.4:7
Liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo,
kila tumwitapo?
K. Bwana ameikumbuka rehema yake, aleluya.
W. Amekuwa mwaminifu kwa nyumba ya Israeli, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Isa.12:5-6
Mwimbieni BWANA; kwa kuwa ametenda makuu; na yajulikane haya katika dunia yote. Paza sauti,
piga kelele, mwenyeji wa Sion; maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
K. Miisho yote ya dunia inastaajabu, aleluya.
W. Imeuona uwezo wa kuokoa wa Mungu wetu, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Tob.14:6-7
Watu wasio Wayahudi wataiacha miungu yao, na watakuja Yerusalemu, na watakaa humo. Na wafalme
wote wa dunia watafurahi katika Yerusalemu, wakimwabudu Mfalme wa Israeli.
K. Rehema na uaminifu vimekutana, aleluya.
W. Haki na amani vimekumbatiana, aleluya.
SALA:
Tuombe: Mungu Baba Mwenyezi, kuzaliwa kwa Mwanao wa Pekee kulikuwa ndio mwanzo wa maisha mapya.
Tunaomba atuopoe katika utumwa wa dhambi. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.