DES. 30 OKTAVA YA NOEL
SALA YA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama ya Yesu, walistaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.
Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu ulioandaa machoni pa watu wote.
Zab.119:1-8 Sheria ya Mungu
Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake(1Yoh.5:3)
Heri watu wanaoishi bila kosa,*
wanaozingatia sheria ya Mungu.
Heri wanaofuata amri zake,*
wanaomtii kwa moyo wote,
ambao hawatendi uovu kamwe;*
bali daima huzingatia mwongozo wake.
Ee Mungu, umetupatia sheria zako*
ili tuzishike kiaminifu.
Laiti mwenendo wangu uimarike,*
kwa kuzishika kanuni zako!
Nikizingatia maagizo yako yote,*
hapo kweli sitaaibishwa.
Nitakusifu kwa moyo mnyofu,*
nikijifunza hukumu zako adilifu.
Nitazishika sheria zako;*
usiniache hata kidogo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.13 Kuomba msaada
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote (Rom.15:13)
Ee Mungu, utanisahau kabisa mpaka lini?*
Utajificha mbali nami mpaka lini?
Mpaka lini nitakuwa na huzuni rohoni mwangu,/
na sikitiko moyoni siku hata siku?*
Mpaka lini adui zangu watafurahia taabu yangu?
Ee Mungu, Mungu wangu;*
uniangalie na kunijibu.
Uniangazie macho yangu,*
nisipatwe na usingizi wa kifo.
Usikubali adui zangu waseme: "Tumemweza huyu!“*
Usiwaache hao wafurahie kuanguka kwangu.
Lakini mimi nautumainia upendo wako mkuu;*
moyo wangu na ufurahie wokovu utokao kwako.
Nitakuimbia wewe, Ee Mungu,*
kwa sababu umenijalia mema.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.14. Uovu wa watu
Pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi (Rom.5:20)
Wapumbavu hujisemea: “Hakuna Mungu."/
Wote ni wafisadi, wametenda mambo ya kuchukiza;*
hakuna atendaye chochote kilicho chema!
Toka mbinguni Mungu awachungulia wanadamu,/
aone kama kuna yeyote mwenye busara,*
kama kuna mtu anayemcha Mungu.
Wote kwa pamoja wamepotoka, wote wameharibika;*
hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.
Mungu asema:*
"Je, wote watendao maovu hawana akili?
Huwakandamiza watu wangu ovyo,/
kama vile watu walavyo mkate;*
wala hawaniombi msaada."
Hapo watatetemeka kwa hofu,*
kwani Mungu awaunga mkono watu waadilifu.
Waovu hupotosha mipango ya mtu mnyonge,*
lakini Mungu ndiye kimbilio lake.
Laiti wokovu umfikie Israeli kutoka Sion!*
Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake,
watu wa Yakobo watashangilia,*
naam, watu wa Israeli watafurahi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama ya Yesu, walistaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.
Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu ulioandaa machoni pa watu wote.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Omb.1:16
Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; Kwa kuwa mfariji yu
mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo
adui ameshinda.
K. Bwana aliwapa joho la furaha.
W. Aliweka taji ya utukufu juu ya vichwa vyao.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Omb.2:11
Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi
Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika
mitaa ya mji.
K. Watakatifu wataishi milele.
W. Bwana mwenyewe ni tuzo lao.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Yer.31:16,17a
Bwana asema hivi: Zuia sauti yako, usilie, na macho yako yasitoke machozi; Maana kazi yako
itapata thawabu, nao watakuja tena toka nchi ya adui; Ndivyo asemavyo BWANA. Tena liko tumaini
kwa siku zako za mwisho, asema BWANA.
K. Watakatifu wafurahie utukufu wao.
W. Na washangilie kwa furaha, na kupumzika.
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, watoto wale Watakatifu walikushuhudia, si kwa kusema, bali kwa kufa:
ujalie imani tunayoitangaza kwa maneno, idhihirishwe kwa matendo. Tunaomba hayo kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.