Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 12 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni mbele ya Bwana, mkiimba kwa furaha.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Peke yangu - wa pili wewe Mungu,
Nasafiri katika njia yangu;
Nihofu nini uwapo karibu,
Mtawala mchana na usiku?
Chini yako ni salama zaidi,
Kuliko kama 'ngelindwa na jeshi.

Saa ya kufa kwangu umepanga,
Mauti yaijua hiyo saa.
Hata 'ngezungukwa na jeshi kali
Halingeshinda nguvu za mauti;
Hazifai kitu kuta za mawe
Unapomtuma wako mjumbe.

Nitaishi kadiri ya amri,
Na kufuata yako maongozi,
Katika amani na utulivu,
Kwani duniani hapana nguvu
Iwezayo kuipokonya roho -.
Yake aliye mkononi mwako.

Ovu lo lote hawezi ogopa,
Mtoto wa Mungu, mteuliwa;
Mambo yetu yote twakuachia,
Lini tuende twangoja sikia.
Watufariji, Mfalme Mkuu,
Wewe Bwana u tumaini letu.

ANT. I: Ee Bwana, uniwezeshe kulitambua pendo lako asubuhi.

Zab.143:1-11 Sala ya kuomba msaada
Mtu hawezi kuwa na uhusiano mwema na Mungu kwa kutii Sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo (Gal.2:16)

Ee Mungu, usikie sala yangu!/
Kwa ajili ya uadilifu wako sikiliza ombi langu!*
Unijibu kwa ajili ya uaminifu wako.

Usinitie mimi mtumishi wako hukumuni,*
maana hakuna mtu aliye mwadilifu mbele yako.

Adui amenifuatia na kunisagasaga kabisa;*
ameniingiza gizani kama mtu aliyekufa zamani.

Nimevunjika moyo kabisa;*
nimekufa ganzi kwa ajili ya woga.

Nakumbuka siku zilizopita;/
natafakari juu ya yote uliyotenda,*
nawaza na kuwazua juu ya matendo yako.

Nanyosha mikono yangu kuomba;*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Ee Mungu, unisikilize hima;*
nimekata tamaa kabisa!

Usijifiche mbali nami,*
nisije nikafanana na wale washukao shimoni.

Asubuhi unijulishe upendo wako mkuu,*
maana nakutumainia wewe.

Nakutolea moyo wangu;*
unioneshe njia ya kwenda.

Uniopoe na adui zangu, Ee Mungu,*
maana nakimbilia kwako.

Unifundishe kutimiza matakwa yako,/
maana wewe ni Mungu wangu!*
Kwa wema wako uniongoze katika njia iliyo sawa.

Uniweke salama, Ee Mungu,/
kwa ajili ya jina lako;*
kwa uadilifu wako, uniokoe taabuni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, uniwezeshe kulitambua pendo lako asubuhi.

ANT. II: Bwana ataleta amani Yerusalemu, amani ifurikayo kama kijito.

WIMBO: Isa.66:10-14a Kitulizo na furaha katika mji mtakatifu
Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu (Gal.4:26)

Furahini pamoja na Yerusalemu,/
Shangilieni kwa ajili yake,*
Ninyi nyote mmpendaye;

furahini pamoja naye kwa furaha,*
ninyi nyote mliao kwa ajili yake;

Mpate kunyonya, na kushibishwa*
kwa maziwa ya faraja zake,

mpate kukama, na kufurahiwa*
kwa wingi wa utukufu wake.

Maana BWANA asema hivi,/
Tazama, nitamwelekezea amani kama mto,*
na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho,

nanyi mtapata kunyonya;*
mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa.

Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji,/
ndivyo nitakavyowafariji ninyi;*
nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu;

Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi,/
na mifupa yenu itasitawi*
Kama majani mabichi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ataleta amani Yerusalemu, amani ifurikayo kama kijito.

ANT. III: Sifa na shangwe kwa Mungu wetu.

Zab.147:1-11 Ni vizuri kumsifu Mungu
Tunakuabudu, Ee Mungu; Ee Bwana, tunakusujudia

Ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa;*
ni vizuri na sawa kabisa kumsifu.

Mungu anaurekebisha mji wa Yerusalemu.*
Anawarudisha salama wakimbizi wake.

Anawaponya waliovunjika moyo;*
anawatibu majeraha yao.

Ameiweka idadi ya nyota,*
na kuzipa kila moja jina.

Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi;*
maarifa yake hayana kipimo.

Mungu huwakweza wanyenyekevu,*
lakini huwatupa waovu mavumbini.

Mwimbieni Mungu nyimbo za shukrani,*
mpigieni kinubi Mungu wetu!

Yeye hulifunika anga kwa mawingu,/
huitengenezea dunia mvua,*
na kuchipusha nyasi vilimani.

Huwapa wanyama chakula chao,*
na kulisha makinda ya kunguru wanaolia.

Yeye hapendezwi na nguvu za farasi,*
wala hafarijiki kwa ushujaa wa askari;

lakini hupendezwa na watu wamchao,*
watu wanaotegemea upendo wake mkuu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Sifa na shangwe kwa Mungu wetu.

SOMO: Rom.8:18-21
Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyafananisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Viumbe vyote vinatazamia kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo, yapo matumaini, maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu.

KIITIKIZANO
K. Mapema asubuhi nitakutafakari, wewe Ee Bwana. (W. Warudie)
K. Umekuwa msaada wangu.
W. Wewe, Ee Bwana.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mapema...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana, uwajulishe watu wako wokovu, na utusamehe dhambi zetu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana, uwajulishe watu wako wokovu, na utusamehe dhambi zetu.

MAOMBI
Ni kusudi lake Baba, kwamba binadamu wamwone yeye katika Mwanae mpenzi. Tumheshimu tukisema:
W. Jina lako litukuzwe.

Kristo ametuletea Habari Njema:
- dunia na ipate kusikia Habari hiyo kwa njia yetu, na hivyo kupata tumaini. (W.)

Tunakusifu na kukushukuru, Bwana wa mbingu na nchi;
- wewe ndiwe tumaini na furaha ya watu, kizazi hata kizazi. (W.)

Ujio wa Kristo uliunde upya Kanisa;
- na ulijalie nguvu na ari katika kuwahudumia watu. (W.)

Tunawaombea Wakristo wanaoteseka kwa ajili ya imani yao:
- uwadumishe katika tumaini lao. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, utujulishe njia ya wokovu, ili, tukishaokolewa kutoka katika mikono ya adui zetu, tukutumikie kiaminifu siku zote za maisha yetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.