Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 12 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Heri wenye moyo safi,
Kwani watamwona Mungu;
Siri ya Bwana ni yao,
Kristo yu rohoni mwao.

Bwana aliacha mbingu,
Uzima, amani kwetu,
Anyenyekee na watu,
Mfano, Mfalme wao.

Tena anajifunua,
Kwayo roho nyenyekevu;
Nao wenye moyo safi,
Takuwa yake makao.

Heri tuitamaniyo
Ni kuwa na Wewe Bwana;.
Tupe moyo mtakatifu
Hekalu utamokaa.

ANT. I: Bwana ni mhisani wangu na kimbilio langu; yeye ndiye ninayemtumainia.

Zab.144 Shukrani kwa ushindi
Ametayarishwa imara kupigana vita, ndio maana ameushinda ulimwengu, na hivi asema, 'Nimeushinda ulimwengu' (Mt. Hilari)

I
Atukuzwe Mungu, mwamba wa usalama wangu,/
aipaye mikono yangu mazoezi ya vita,*
na kuvifunza vidole vyangu mapambano.

Yeye ndiye kinga yangu amini,*
ngome yangu, usalama wangu na mwokozi wangu.

Yeye ni ngao yangu ninayotegemea;*
huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu.

Ee Mungu, mtu ni nini hata umwangalie?*
Mwanadamu ni nini hata umkumbuke?

Binadamu ni kama pumzi tu;*
siku zake ni kama kivuli kipitacho.

Ee Mungu, pasua mbingu ushuke!*
Uiguse milima, nayo itoe moshi!

Lipusha umeme, uwatawanye adui;*
upige mishale yako, uwahangaishe!

Unyoshe mkono wako kutoka juu,*
uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi;

uniopoe katika makucha ya wageni,/
ambao maneno yao yote ni ya uwongo,*
na hushuhudia uwongo kwa kiapo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana ni mhisani wangu na kimbilio langu; yeye ndiye ninayemtumainia.

ANT. II: Wamebarikiwa watu ambao Bwana ndiye Mungu wao.

II
Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya;*
nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi,

wewe uwapaye wafalme ushindi,*
na kumwokoa Daudi, mtumishi wako!

Uniepushe na upanga wa adui katili;*
uniopoe katika makucha ya wageni,

ambao maneno yao yote ni ya uwongo,*
na hushuhudia uwongo kwa kiapo.

Naam, wana wetu katika ujana wao,*
Wawe kama mimea inayokua vizuri.

Binti zetu wawe kama nguzo za pembeni,*
zilizochongwa vizuri ili kupamba Hekalu.

Ghala zetu zijae mazao ya kila aina.*
Kondoo wetu mashambani wazae maelfu na maelfu.

Mifugo yetu iwe na afya na nguvu;/
isitupe mimba wala kuzaa kabla ya wakati.*
Kusiwepo tena udhalimu katika mitaa yetu.

Heri taifa ambalo limejaliwa hayo!*
Heri taifa ambalo Mungu wao ni Mungu!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wamebarikiwa watu ambao Bwana ndiye Mungu wao.

ANT. III: Sasa Mungu wetu amejipatia ushindi na utawala.

WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-12a Hukumu ya Mungu
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!

Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!

Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.

Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,

watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.

Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!

Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu

akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.

Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwanakondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;

maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.

Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Sasa Mungu wetu amejipatia ushindi na utawala.

SOMO: Kol.1:23
Mnapaswa, lakini, kuendelea kuwa amini juu ya msingi imara na thabiti, na msikubali kutikiswa kutoka tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili, Injili ambayo imekwisha hubiriwa kwa kila mtu duniani.

KIITIKIZANO
K. Bwana ni mchungaji wangu; sitapungukiwa na kitu. (W. Warudie)
K. Hunilaza katika malisho ya majani mabichi.
W. Sitapungukiwa na kitu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Bwana amewashibisha mema, wenye njaa na kiu ya haki.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana amewashibisha mema, wenye njaa na kiu ya haki.

MAOMBI
Nuru huangaza gizani, nalo giza haliwezi kushinda. Tumshukuru Bwana wetu kwa kutujalia mwanga wake katika maisha yetu.
W. Bwana Yesu Kristo, wewe ndiwe nuru yetu.

Neno wa Mungu, umeleta mwanga wa milele katika dunia iliyojaa giza:
- kwa mwanga huo, fungua akili na mioyo ya waamini wako wote. (W.)

Watunze wote wanaotolea maisha yao kuwahudumia wengine:
- neema yako iyaongoze matendo yao, nao waimarike mpaka mwisho. (W.)

Bwana, ulimponya yule aliyepooza, ukamsamehe dhambi zake:
- utuondolee hatia zetu zote, na utuponye majeraha ya dhambi zetu. (W.)

Binadamu hufuata mwanga uwaongozao kwenye elimu mpya na uvumbuzi:
- uwawezeshe kutumia vipawa vyao kwa manufaa ya watu wote, na hivi wakutukuze. (W.)

Uwaondoe wafu kutoka gizani na kuwaingiza katika mwanga wako wa ajabu:
- kwa huruma yako, uwaoneshe mng'ao wa utukufu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tumwombe Baba, kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, yasikilize kwa wema masifu yetu ya jioni, na utujalie, tukifuata mfano wa Mwanao, saburi, tuweze kutoa mapato mazuri kwa kazi zetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.