Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 12 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Kama wanipenda, shika amri zangu, asema Bwana.

Zab.119:153-160 XX Kuomba msaada
Uangalie mateso yangu, uniokoe,*
kwa maana sikusahau sheria yako.

Unitetee na kunikomboa;*
unisalimishe kama ulivyoahidi.

Waovu hawataokolewa,*
maana hawazijali kanuni zako.

Huruma yako ni kubwa, Ee Mungu;*
Unijalie uhai kama ulivyoahidi.

Adui na wadhalimu wangu ni wengi,*
lakini mimi sikiuki maagizo yako.

Niwaonapo wahaini hao nachukizwa mno,*
kwa sababu hawazishiki amri zako.

Tazama, Ee Mungu, jinsi nizipendavyo amri zako!*
Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu.

Kitovu cha sheria yako ni ukweli,*
hukumu zako za haki, zote ni za milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kama wanipenda, shika amri zangu, asema Bwana.

ANT. II: Bwana na akubariki, ili uwe na amani siku zote za maisha yako.

Zab.128 Tuzo kwa jamaa imchayo Mungu
'Bwana akubariki kutoka Sion,' yaani kutoka Kanisa lake (Arnobius)

Heri wote wamchao Mungu,*
wanaoishi kufuatana na amri zake.

Kazi zako zitakupatia mahitaji yako,*
utaona furaha na kufanikiwa.

Mke wako atakuwa kama mzabibu*
wenye matunda mengi nyumbani mwako;

watoto wako watakuwa kama machipukizi*
ya mizeituni kuizunguka meza yako.

Naam, ndivyo atakavyobarikiwa*
mtu amchaye Mungu.

Mungu akubariki toka Sion!/
Uione fanaka ya Yerusalemu,*
siku zote za maisha yako.

Uishi na hata uwaone wajukuu wako!*
Amani iwe na Israeli!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana na akubariki, ili uwe na amani siku zote za maisha yako.

ANT. III: Bwana atakuangamizia adui zako.

Zab.129 Sala dhidi ya adui za Israeli
Kanisa lasimulia mateso linayovumilia (Mt. Augustino)

Israeli anasema:/
"Mara nyingi adui wamenitesa,*
tangu ujana wangu!

Naam, wamenitesa tangu ujana wangu,*
lakini hawakuweza kunishinda.

Walinikatakata mgongoni mwangu,*
waliufanya kama shamba lililolimwa.

Lakini Mungu ni mwadilifu;*
amezikata kamba za hao waovu.“

Waaibishwe na kushindwa kabisa*.
wote wale wauchukiao mji wa Sion.

Wote wafanane na nyasi juu ya paa la nyumba,*
ambazo hunyauka kabla hazijakua;

hakuna anayejishughulisha kuzikusanya,*
wala kuzichukua kama matita.

Hakuna apitaye karibu atakayewaambia:/
"Mungu awabariki!*
Twawabariki kwa jina la Mungu.“

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana atakuangamizia adui zako.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Yoh.3:23-24
Amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru. Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia sisi, twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.

K. Wewe, Bwana, wamtunza mtu aliye mwadilifu.
W. Wewe, Ee Mungu, wajaribu mioyo na mawazo.

SALA:
Tuombe: Bwana, wewe ambaye saa hii uliwajalia Roho Mtakatifu mitume walipokuwa wakisali, utujalie nasi neema hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Hek.1:1-2
Pendeni haki, enyi waamuzi wa dunia; Tafakarini habari za BWANA kwa moyo mwema; na kumtafuta katika unyofu wa moyo. Kwa sababu huonekana nao wasiomjaribu, na kufunuliwa kwao wasiokosa kumwamini.

K. Umtumainie Bwana, ukatende mema.
W. Ndipo utamiliki nchi, na kuwa salama.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, wewe ni mwanga mtupu, na ndani yako hamna giza. Nuru yako, kwa mng'aro wake wote, ituangaze, ili tuweze kufuata kwa furaha amri zako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Ebr.12:1b-2
Tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung'ang'ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.

K. Moyo wangu wamngojea Bwana.
W. Nalitumainia neno lake.

SALA:
Tuombe: Bwana, twakuomba utujalie tuweze kuvumilia taabu na magumu kama alivyovumilia Mwanao wa pekee, anayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.