ALHAMISI JUMA 12 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 2Fal.24:8-17
Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi. Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maakida wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli. Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli. Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.79:1-5,8-9(K)9
1. Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako,
Wamelinajisi hekalu lako takatifu.
Wamefanya Yerusalemu chungu ngungu,
Wameziacha maiti za watumishi wako.
Ziwe chakula cha ndege wa angani.
Na miili wa watauwa wako
Iwe chakula cha wanyama wa nchi.

(K) Utuokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako.

2. Wamemwaga damu yao kama maji
Pande zote za Yerusalemu,
Wala hapakuwa na mzishi.
Tumekuwa lawama kwa jirani zetu,
Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele?
Wivu wako utawaka kama moto? (K)

3. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima.
Kwa maana tumedhilika sana. (K)

4. Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughfiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)

SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!

INJILI: Mt.7:21-29
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako hutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejinga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa. Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.