Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni, tumwabudu Bwana, kwani yeye ni Mungu wetu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Fahari yake ye Baba
Kristo nuru yetu,
Kwa upendo na huruma
Aja kufanya kivuko
Cha shimo kubwa ajabu,
Shimo kubwa la madhambi
Baina ya wanadamu
Na Mungu Mtakatifu.

Kristo siku ya jana,
Na leo pia Kristo,
Ana hali ile ile,
Habadiliki milele,
Mfano wa Mungu wetu,
Mungu aliyefichika;
Na 'Hekima ya Milele'
Ndilo hasa jina lake.

Neno lake hulishika
Karne hata karne,
Yupo pamoja na sisi
Hadi mwisho wa nyakati;
Mchana Yeye ni wingu,
Usiku mwali wa moto,
Hivyo hututangulia
Katika zakeye njia.

Tunakutukuza Baba
Chanzo halisi cha mwanga,
Kadhalika na Kristo,
Yeye Mwanao mpendwa,
Akaaye ndani yetu
Pamoja na Roho wako:
Ndo Utatu wa milele
Katika Mungu Mmoja.

ANT. I: Matukufu yasemwa juu yako, Ee Mji wa Mungu.

Zab.87 Sifa ya Yerusalemu
Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu (Gal.4:26)

Mungu amejenga mji Sion,*
juu ya milima mitakatifu.

Mungu anaupenda Sion,*
kuliko makao mengine ya Yakobo.

Sikiliza, Ee mji wa Mungu,*
mambo ya fahari yasemwayo juu yako:

"Katika orodha ya wanijuao,*
wapo watu wa Misri na Babuloni.

Watu wa Filistia, Turo na Ethiopia*
watakuwa miongoni mwao."

Lakini juu ya Sion itasemwa kwamba/
watu wote wamezaliwa huko,*
na Mungu Mkuu ndiye aliyeuthibitisha.

Mungu atakapoorodhesha mataifa,/
ataandika juu ya kila mmoja: *
'Huyu amezaliwa mjini Sion!'

Wanaimba na kucheza ngoma:*
“Limbuko letu ni kwako Sion.”

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;*
utukufu wako uenee duniani kote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Matukufu yasemwa juu yako, Ee mji wa Mungu.

ANT. II: Bwana anakuja akiwa na uwezo; amepata tuzo kwa ushindi wake.

WIMBO: Isa.40:10-17 Mchungaji Mwema: Mungu mkuu na mwenye hekima yote
Naja upesi, pamoja na tuzo (Ufu.22:12)

Tazameni, Bwana MUNGU atakuja kama shujaa,*
Na mkono wake ndio utakaomtawalia;

Tazameni, thawabu yake i pamoja naye,*
Na ijara yake i mbele zake.

Atalilisha kundi lake kama mchungaji,*
Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake,

Na kuwachukua kifuani mwake.*
Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Ni nani aliyeyapima maji*.
Kwa konzi ya mkono wake,

Na kuzikadiri mbingu kwa shubiri,*
Na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi,

Na kuipima milima kwa uzani,*
Na vilima kama kwa mizani?

Ni nani aliyemwongoza roho ya BWANA,*
Na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake?

Alifanya shauri na nani,/
Ni nani aliyemwelimisha*
Na kumfunza njia ya hukumu,

Na kumfunza maarifa,*
Na kumwonesha njia ya fahamu?

Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo,*
Huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani;

Tazama, yeye huvinyanyua visiwa*
Kama ni kitu kidogo sana.

Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni,*
Wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara.

Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake;/
Huhesabiwa kwake kuwa duni*
Na si kitu, na ubatili.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana anakuja akiwa na uwezo; amepata tuzo kwa ushindi wake.

ANT. III: Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, mkasujudu mbele ya mlima wake mtakatifu.

Zab.99 Mungu mfalme mkuu
Wewe u mkuu zaidi kuliko Makerubi; ulibadilisha hali ya ulimwengu, pale ulipojichukulia hali yetu ya kibinadamu (Mt. Athanasius).

Mungu anatawala,*
mataifa yanatetemeka!

Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa,*
nayo dunia inatikisika!

Mungu ni mkuu katika Sion;*
ametukuka juu ya mataifa yote.

Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha.*
Mtakatifu ndiye yeye!

Ee Mfalme mkuu, mpenda uadilifu!/
Umethibitisha haki katika Israeli;*
umeleta uadilifu na haki.

Msifuni Mungu, Mungu wetu;/
angukeni kifudifudi mbele yake.*
Mtakatifu ndiye yeye!

Musa na Aroni walikuwa makuhani wake;/
Samweli alikuwa miongoni mwa waliomlilia;*
walimlilia Mungu, naye akawasikiliza.

Alisema nao katika mnara wa wingu;*
walizitii sheria na amri alizowapa.

Ee Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza;/
uliwaonesha kuwa wewe ni Mungu anayesamehe,*
ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao.

Msifuni Mungu, Mungu wetu;/
abuduni katika mlima wake mtakatifu!*
Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, mkasujudu mbele ya mlima wake mtakatifu.

SOMO: 1Pet.4:10-11
Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo.

KIITIKIZANO
K. Naliita kwa moyo wangu wote: Bwana nisikie. (W. Warudie)
K. Nitazitii amri zako.
W. Bwana nisikie.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Naliita...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Tumtumikie Bwana kwa uchaji, naye atatuopoa mikononi mwa adui zetu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tumtumikie Bwana kwa uchaji, naye atatuopoa mikononi mwa adui zetu.

MAOMBI
Tunamwabudu na kumtukuza Mungu wetu anayetawala juu mbinguni. Yeye ni Bwana wa vyote, na ulimwengu wote ni kama si kitu mbele yake.
W. Tunakuabudu, Bwana wetu na Mungu wetu.

Baba wa milele, kwa nguvu zako tu ndio tunaweza kukusifu:
- kuumbwa kwetu ni kwa ajabu, lakini fahari na furaha ya wokovu wetu katika Kristo ni kubwa zaidi. (W.)

Bwana, uwe nasi tunapoanza siku hii mpya:
- fanya mioyo yetu ikutafute, na utashi wetu ukutumikie. (W.)

Utujalie tuhisi zaidi uwepo wako:
- utuwezeshe kuwa na heshima na upendo kwa viumbe vyako. (W.)

Kukujua Wewe ni kuvipenda viumbe vyako:
- utujalie tuweze kuwahudumia ndugu zetu, kwa kazi na maisha yetu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi, unayeishi milele, uwaangazie kwa nuru ya utukufu wako watu wanaoishi katika uvuli wa mauti, kama ulivyofanya zamani, pale Bwana wetu Yesu Kristo, Jua la Haki, alipotujia kutoka juu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.