Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 15 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT. I: Unitegemeze kwa ahadi yako, Bwana, nami nitaishi.

Zab.119:113-120 XV Usalama katika sheria ya Mungu
Nawachukia watu wasioaminika kwako,*
lakini naipenda sheria yako.

Wewe ni mlinzi wangu na ngao yangu;*
nategemea sana neno lako.

Ondokeni kwangu, enyi waovu,*
ili nipate kushika maagizo ya Mungu wangu.

Unipe nguvu ulivyoahidi, nami nitaishi;*
usikubali niaibike, tumaini langu.

Unitegemeze, niwe salama;*
niwe daima msikivu kwa kanuni zako.

Unawakataa wote wanaokiuka kanuni zako;*
mawazo yao maovu ni ya bure.

Waovu wote wawaona kuwa takataka,*
kwa hiyo mimi napenda maagizo yako.

Natetemeka kwa hofu kwa sababu yako;*
nimejaa hofu kwa sababu ya hukumu zako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Unitegemeze kwa ahadi yako, Bwana, nami nitaishi.

ANT. II: Uje utusaidie, Ee Mungu mwokozi wetu, na utusamehe dhambi zetu.

Zab.79:1-5,8-11,13 Wakati wa maafa ya taifa
Ingekuwa afadhali kama wewe pia ungeelewa leo hii ujumbe wa amani (Lk.19:42)

Ee Mungu, watu wasiokujua wameivamia nchi yako./
Wamelichafua Hekalu lako takatifu,*
na kuufanya magofu mji wa Yerusalemu.

Wameacha maiti za watumishi wako ziliwe na ndege,*
miili ya watu wako iwe chakula cha wanyama wa porini.

Damu yao imemwagwa kama maji mjini Yerusalemu,*
wamelazwa humo na hakuna wa kuwazika.

Tumekuwa aibu kwa mataifa jirani,*
jirani zetu wanatucheka na kutudhihaki.

Ee Mungu, je, utakasirika hata milele?*
Hasira yako itawaka kama moto hata lini?

Usituadhibu kwa sababu ya makosa ya wazee wetu.*
Huruma yako itujie hima, tumekandamizwa mno!

Utusaidie, Ee Mungu, mwokozi wetu,*
kwa heshima ya jina lako.

Utuokoe na kutusamehe dhambi zetu,*
kwa ajili ya jina lako.

Kwa nini mataifa yatuambie: “Yuko wapi Mungu wenu?"/
Utujalie kuona ukiwaadhibu watu wa mataifa,*
kwa vile wamemwaga damu ya watumishi wako.

Kilio cha hao waliofungwa kikufikie;*
kwa nguvu yako uwaokoe waliohukumiwa kufa.

Nasi watu wako, tulio kondoo wa kundi lako,*
tutakushukuru milele, na kukusifu nyakati zote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Uje utusaidie, Ee Mungu mwokozi wetu, na utusamehe dhambi zetu.

ANT. III: Ee Mungu wa majeshi, utuangalie kutoka mbinguni, na uje kuutazama huu mzabibu wako.

Zab.80 Kwa ajili ya urekebisho wa Israeli
Njoo, Bwana Yesu (Ufu.22:20)

Utusikilize, ewe Mchungaji wa Israeli,/
unayewaongoza watu wako, Yosefu, kama kondoo.*
Ewe ukaaye juu ya viumbe vyenye mabawa,

ujioneshe kwa Efraimu, Benyamini na Manase.*
Uoneshe nguvu yako, uje ukatuokoe!

Uturekebishe, Ee Mungu;*
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.

Ee Mungu, Mungu mwenye nguvu,*
hata lini utazikasirikia sala za watu wako?

Umefanya huzuni iwe chakula chetu;*
umetunywesha machozi kwa wingi.

Umetufanya kisa cha ubishi kwa jirani zetu;*
adui zetu wanatudhihaki.

Ee Mungu mwenye nguvu, uturekebishe,*
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.

Ulileta mzabibu mmoja kutoka Misri;/
ukawafukuza watu wa mataifa mengine,*
na kuupanda katika nchi yao.

Uliupalilia upate kukua,*
nao ukatoa mizizi, ukaenea kote nchini.

Uliifunika milima kwa kivuli chake,*
na matawi yake yakawa kama mierezi mikubwa.

Matawi yake yalienea mpaka baharini;*
machipukizi yake mpaka kando ya mto Eufrate.

Mbona ulibomoa kuta zilizouzunguka?*
Sasa kila apitaye anachuma zabibu zake;

nguruwe - mwitu wanauharibu,*
na wanyama wa porini wanautafuna!

Ee Mungu mwenye nguvu, utugeukie tena!*
Uangalie toka mbinguni, uutunze mzabibu huo.

Uulinde huo mche ulioupanda kwa mkono wako;*
hicho kichipukizi ulichokisitawisha.

Watu walioukata na kuuteketeza,*
uwatazame kwa ukali, waangamie.

Mkono wako umkinge huyo uliyemfadhili;*
huyo uliyemteua kwa ajili yako.

Hatutakuacha na kukuasi tena;*
utujalie uzima, nasi tutakusifu.

Ee Mungu, Mungu mwenye nguvu, uturekebishe;*
utuangalie kwa wema, nasi tutasalimika.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Ee Mungu wa majeshi, utuangalie kutoka mbinguni, na uje kuutazama huu mzabibu wako.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Hek.19:22
Wewe, BWANA, katika yote uliwakuza watu wako, Ukawatukuza wala hukuwadharau, Ukasimama upande wao kila wakati kila mahali.

K. Wewe ndiwe Mungu mwenye kutenda maajabu.
W. Umewajulisha watu uwezo wako.

SALA:
Tuombe: Bwana, wewe ambaye saa hii uliwajalia Roho Mtakatifu mitume walipokuwa wakisali, utujalie nasi neema hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kum.4:7
Liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo?

K. Bwana yu karibu na wale wamwitao.
W. Naye atazisikiliza sala zao.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, wewe ni mwanga mtupu, na ndani yako hamna giza. Nuru yako, kwa mng'aro wake wote, ituangaze, ili tuweze kufuata kwa furaha amri zako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Esta 10:9
Na taifa langu ni Israeli, waliomlilia Mungu wakaokoka. Maana Mungu amewaokoa watu wake na kutuopoa katika maovu hayo yote, Bwana amefanya ishara kuu na mambo ya ajabu yasiyofanyika katikati ya mataifa.

K. Ee Bwana, nitakutukuza kwa kuwa umesikiliza sala yangu.
W. Umekuwa mwokozi wangu.

SALA:
Tuombe: Bwana, twakuomba utujalie tuweze kuvumilia taabu na magumu kama alivyovumilia Mwanao wa pekee, anayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.