ALHAMISI JUMA 18 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Yer.31:31-34
Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.51:10–13,16-17(K)10
1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho wako mtakatifu usiniondolee.

(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

2. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe kuridhi sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliyovunika na kupondeka,
Ee Mungu, hutadharau. (K)

SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!

INJILI: Mt.16:13-23
Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simony Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. Ndipo aliwakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo. Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazia yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.