ALHAMISI JUMA 1 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Est.4:17
Malkia Esta naye alimkimbilia Bwana, akishikwa na uchungu wa mauti. Akazivua nguo zake za fahari akavaa nguo za huzuni, na kilio, na badala ya manukato mazuri alijitia majivu na samadi kichwani; akajinyenyekesha mwili wake, hata mahali pa mapambo ya furaha alijifunika kwa nywele zake zilizofumuliwa. Akamwomba Bwana wa Israeli, akisema: Bwana wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila Wewe; maana hatari yangu imo mkononi mwangu. Tangu nilipozaliwa katika kabila ya jamaa yangu, nimesikia ya kuwa Wewe, Bwana, ulimchagua Israeli katika mataifa yote, na baba zetu katika jamaa zao, kuwa urithi wa daima, ukawatimilizia yote uliyoyaahidi. Utukumbuke, Ee Bwana; ujifunue wakati wa taabu yetu; unipe moyo thabiti, Ee Mfalme wa miungu na Bwana wa milki zote. Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuza moyo wake apate kumchukia yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye. Lakini utuokoe sisi kwa mkono wako; unisaidie mimi niliye peke yangu, bila msaidizi mwingine ila Wewe, Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.138:1-3,8-9
1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
Nitalishukuru jina lako.

(K) Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.

2. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)

3. Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Bwana atanitimilizia mambo yangu;
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)

SHANGILIO: Eze.33:11
Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu,
asema Bwana,
Bali aiache njia yake mbaya, akaishi.

INJILI: Mt.7:7-12
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akiomwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hivyo ndiyo torati na manabii.

MAOMBI
Ndugu, sala ni muhimu kwa ajili ya kupata mahitaji yetu ya kimwili na kiroho. Katika mfungo huu wa Kwaresima tunahimizwa sana kusali, ili kuyashinda maovu ya shetani. Kwa hiyo tuombe. Ee Mungu, twakuomba:

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Viongozi wetu wa dini watoe daima mfano mwema kwa kuishi maisha ya sala siku zote.

2. Sala iwe kinga yetu dhidi ya vishawishi na maovu ya aina yoyote.

3. Uwaepushe waamini wako na mila potovu za kutambika au kutolea sadaka kwa mahoka na miungu ya uwongo.

4. Bila kuchoka, tunawaombea marehemu wetu, ili waokoke na kupata uzima wa milele.

Hayo ni baadhi tu ya yale tunayoyahitaji. Utujalie mahitaji yetu kadiri ya mapenzi yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.