Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI

ANTIFONA YA MWALIKO:
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

Ant. ya Mwaliko
Tumwabudu Bwana, mfalme atakayekuja.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Sikieni sauti ya mjumbe
'Kristo yu karibu', yasema,
'Tupieni mbali za giza ndoto,
Na mkaribisheni Kristo,
Yeye aliye nuru ya mchana!'

Roho iloshikana na dunia
Iamshwe na hilo onyo kali;
Yesu Kristo ni lake jua,
Liondoalo ulegevu wote,
Asubuhi uwinguni hung'aa.

Basi na atakapokuja tena
Kwa utukufu na vitisho vingi,
Na kuifunika hofu dunia,
Na atokee katika mawingu
Aje na kuwa wetu mtetezi.

ANT. I: Kinanda na kinubi, amkeni; nitaiamsha alfajiri.

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii hutukuza mateso ya Kristo (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

Wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;*
utukufu wako uenee duniani kote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kinanda na kinubi, amkeni; nitaiamsha alfajiri.

ANT. II: Bwana asema hivi: Watu wangu watashibishwa mema yangu.

WIMBO: Yer.31:10-14 Furaha ya watu waliokombolewa
Yesu ilimpasa kufa kusudi awaunganishe watoto wa Mungu waliokuwa wametawanyika (Yoh.11:51-52)

Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa,*
litangazeni visiwani mbali; mkaseme,

Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda,*
kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo,*
amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.

Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sion,*
wataukimbilia wema wa BWANA,

nafaka, na divai na mafuta,*
na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe;

na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji;*
wala hawatahuzunika tena kabisa.

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,*
na vijana na wazee pamoja;

maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,/
nami nitawafariji, na kuwafurahisha*
waache huzuni zao.

Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono,*
na watu wangu watashiba kwa wema wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana asema hivi: Watu wangu watashibishwa mema yangu.

ANT. III: Bwana ni mkuu, astahili sifa katika mji wa Mungu wetu.

Zab.48 Sion mji wa Mungu
Akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, yaani Yerusalemu (Ufu.21:10)

Mungu ni mkuu na wa kusifika sana,/
katika mji wa Mungu wetu,*
juu ya mlima wake mtakatifu.

Sion, mlima wa Mungu, ni mrefu na mzuri;*
mji wa mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu.

Katika ngome za mji Sion,*
Mungu amejionyesha kuwa mwamba wa usalama.

Wafalme walikusanyika,*
wakaanza kushambulia.

Lakini walipouona tu mji wa Sion, wakashangaa;*
akashikwa na hofu, wakatimua mbio.

Woga uliwashika wakaanza kuhangaika,*
wakawa kama mwanamke anayejifungua.

Uliwarusharusha kama meli katika dhoruba./
Yote tuliyosikia Mungu ametenda,*
sasa sisi wenyewe tumeyaona;

katika mji wa Mungu, Mungu mwenye nguvu,*
Mungu atauweka mji huo salama milele.

Ee Mungu, twautafakari upendo wako mkuu,*
tukiwa Hekaluni mwako.

Wewe wasifika kila mahali,/
sifa zako zaenea popote duniani.*
Wewe watawala kwa haki;

watu wa Sion wafurahi!/
Wewe watoa hukumu zilizo sawa;*
watu wa mji wa Yuda na washangilie!

Haya, nendeni Sion mkauzunguke,*
nendeni mkahesabu minara yake.

Zitazameni kuta zake na kuchunguza ngome zake;*
mpate kukisimulia kizazi kijacho, kwamba:

“Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele!*
Atakuwa kiongozi wetu milele"!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana ni mkuu, astahili sifa katika mji wa Mungu wetu.

SOMO: Isa.45:8
Dondokeni, enyi mbingu, toka juu; mawingu na yamwage haki. Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, BWANA, nimeiumba.

KIITIKIZANO
K. Utukufu wa Bwana utakung'aria, Ee Yerusalemu. Kama jua Bwana atachomoza juu yako. (W. Warudie)
K. Utukufu wake utajitokeza katikati yako.
W. Kama jua Bwana atachomoza juu yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utukufu wa Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Nitamngoja Bwana, mwokozi wangu. Nitamtumainia yeye, maana yu aja, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Nitamngoja Bwana, mwokozi wangu. Nitamtumainia yeye, maana yu aja, aleluya.

MAOMBI
Mbingu zifunguke, na mawingu yammimine mwenye haki; azaliwe duniani Kristo, ambaye ni hekima na nguvu ya Mungu.
W. Bwana, uwe karibu nasi leo.

Bwana Yesu Kristo, umetualika kushiriki ufalme wako;
- utuwezeshe kuingia katika ufalme huo, na kuishi kadiri ya mwito wako. (W.)

Ulimwengu haukujui:
- kwa njia yetu sisi, jioneshe kwa watu wote. (W.)

Tunakushukuru, Bwana, kwa yote tuliyo nayo:
- utupe moyo wa kutoa msaada kwa wenye dhiki. (W.)

Tunautazamia ujio wako, Bwana Yesu:
- utakapopiga hodi, utukute tunasali na kusifu kwa furaha. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana, uje na utuoneshe uwezo wako. Uje, kwa uwezo wako mkuu, kutusaidia. Uwe na huruma, na utusamehe dhambi zetu, ambazo ndizo zinazochelewesha wokovu wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.