ALHAMISI JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.
Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.
Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB
ANT. I: Ee Bwana, nilikuomba msaada, nawe umeniponya.
Nitakushukuru milele.
Zab.30 Sala ya Shukrani
Kristo, baada ya ufufuko wake mtukufu, amshukuru Baba yake (Kasiani)
Nakusifu, Ee Mungu, maana umeniokoa,*
wala hukuwaacha adui zangu wanisimange.
Ee Mungu, Mungu wangu,*
nilikulilia, nawe ukaniponya.
Ee Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu;*
umenitoa katika msafara wa waendao Shimoni.
Mwimbieni Mungu sifa, enyi watakatifu wake;*
kumbukeni utakatifu wake na kumsifu.
Hasira yake hudumu kitambo kidogo,*
lakini fadhili yake hudumu milele.
Kilio huwapo jioni,*
lakini asubuhi husikika sauti ya furaha.
Mimi katika usitawi wangu, nilisema:*
"Kamwe sitatikisika!"
Ee Mungu, kwa fadhili yako,*
umeniimarisha kama mlima mkubwa.
Lakini ukajificha mbali nami,*
nami nikaogopa.
Nilikulilia wewe, Ee Mungu;*
nilikusihi wewe Mungu:
“Je, nikifa utapata faida gani?*
Kuna faida gani nikishuka Shimoni?
Je, waliokufa wanaweza kukusifu?*
Je, wanaweza kutangaza wema wako mkuu?
Usikie, Ee Mungu, unihurumie,*
Ee Mungu, unisaidie!"
Wewe umegeuza ombolezo langu*
kuwa ngoma ya furaha;
umeniondolea huzuni yangu,*
ukanijalia furaha tele tele.
Basi, sitakaa kimya,*
bali nitakuimbia sifa.
Ee Mungu, Mungu wangu,*
nitakushukuru milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Ee Bwana, nilikuomba msaada, nawe umeniponya.
Nitakushukuru milele.
ANT. II: Heri mtu yule, ambaye Mungu anamwona hana dhambi.
Zab.32 Maondoleo ya dhambi
Daudi asema, ana heri yule ambaye Mungu amemfanya awe na uhusiano mwema naye bila
kujali matendo yake (Rom.4:6)
Heri yao waliosamehewa dhambi zao,*
ambao makosa yao yameondolewa.
Heri yake mtu aliyesamehewa kosa na Mungu,*
mtu ambaye hana hila moyoni mwake.
Wakati nilipokuwa sijakiri makosa yangu,*
nilikuwa nimedhoofika kwa kulia mchana kutwa.
Mchana na usiku uliniadhibu, Ee Mungu;/
nikafyonzwa nguvu zangu,*
kama maji wakati wa kiangazi.
Kisha nikaziungama dhambi zangu kwako;*
wala sikuuficha uovu wangu.
Niliazimu kukiri makosa yangu kwako, Ee Mungu;*
ndipo nawe ukanisamehe dhambi zangu.
Kwa hiyo, kila mcha Mungu, akuombe wakati wa shida;*
yakitokea mafuriko ya taabu hayatamfikia.
Wewe ndiwe kimbilio langu;/
wewe wanilinda katika taabu.*
Nimejawa shangwe maana umenikomboa.
Mungu asema, "Nitakuonesha njia ya kufuata.*
Nitakufundisha na kukuelekeza.
Usiwe mpumbavu kama farasi au nyumbu,*
wasiotawalika ila kwa lijamu na hatamu."
Watu waovu watapata mateso mengi;/
lakini wanaomtumaini Mungu*
wanalindwa kwa upendo wake mkuu.
Enyi waadilifu, furahieni na kushangilia/
aliyotenda Mungu;*
enyi mlio wanyofu, pigeni vigelegele vya furaha.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Heri mtu yule, ambaye Mungu anamwona hana dhambi.
ANT. III: Bwana amempa mamlaka, heshima na milki; na watu wote watamtumikia.
WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-1
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!
Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!
Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.
Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,
watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.
Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!
Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu
akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.
Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwanakondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;
maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.
Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Bwana amempa mamlaka, heshima na milki; na watu wote
watamtumikia.
SOMO: Yak.5:7-8,9b
Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa
subira mimea yake itoe mavuno mazuri. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. Nanyi
pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia.
Hakimu yu karibu, tayari kuingia.
KIITIKIZANO
K. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe. (W. Warudie)
K. Utuoneshe uso wa tabasamu, nasi tutakuwa salama.
W. Njoo kwetu, utuokoe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana, Mungu...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mzao wako amebarikiwa.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mzao wako amebarikiwa.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, Nuru kuu, ambaye manabii waliahidi kwamba atawaangazia wale walio katika kivuli cha mauti.
W. Njoo, Bwana Yesu!
Unawaangaza watu wote,
- ifungue mioyo ya watu wako, iwe wazi kwa wote. (W.)
Mwana wa Mungu, katika wewe twamwona Baba,
- uje utuoneshe maana halisi ya upendo wa kweli. (W.)
Kristo Yesu unatujia katika hali ya ubinadamu,
- uwezeshe mapokezi tunayokufanyia yatufanye wana wa Mungu.
(W.)
Waifungua milango ya uhuru na uzima,
- uwafikishe marehemu kwenye uhuru wa milele. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tumwombe Baba, kwa maneno yale aliyotufundisha
Mwokozi wetu: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana, uje na utuoneshe uwezo wako. Uje, kwa uwezo wako mkuu, kutusaidia. Uwe na huruma na
utusamehe dhambi zetu, ambazo ndizo zinazochelewesha wokovu wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya
Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.