Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 1 MAJILIO
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

Zab.119:17-24 III Furaha katika sheria ya Mungu
Unifadhili mimi mtumishi wako,*
nipate kuishi na kushika agizo lako.

Uyafumbue macho yangu,*
niyaone maajabu ya sheria yako.

Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani;*
usinifiche maagizo yako.

Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa*
ya kutaka kujua daima hukumu zako.

Wewe wawakemea watu wenye kiburi;*
walaaniwe wanaokiuka amri zako.

Uniepushe na matusi na madharau yao,*
maana nimezishika kanuni zako.

Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu,*
mimi mtumishi wako nitajifunza maagizo yako.

Amri zako ni furaha yangu;*
hunipa ushauri mwema.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.25 Kuomba uongozi na ulinzi
Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa (Rom.5:5)

I
Kwako naja, Ee Mungu, kwa moyo wangu wote!*
Nakutumainia wewe, Ee Mungu wangu,

usiniache niaibike;*
adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.

Wote wale wakutegemeao hawataaibika;*
lakini wanaokuasi ovyo wataaibika.

Ee Mungu, unijulishe njia yako;*
naam, unipe mwongozo wako.

Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,/
kwani wewe ni Mungu unayeniokoa;*
ninakutumainia wewe daima.

Ee Mungu, uukumbuke wema wako mkuu;/
uukumbuke na upendo wako mkuu,*
maana vimekuwako tangu milele.

Unisamehe dhambi na makosa ya ujana wangu;/
unikumbuke kadiri ya upendo wako mkuu,*
kwa ajili ya wema wako, Ee Mwenyezi.

Mungu ni mwema na mwadilifu;*
huwapa wakosefu mwongozo.

Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;*
naam, huwafundisha hao njia yake.

Mungu huwalinda kwa upendo mkuu na uaminifu,*
wale wanaozingatia matakwa ya agano lake.

Kwa heshima ya jina lako, Ee Mungu,*
unisamehe uovu wangu, kwani ni mkubwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Kila mtu anayemcha Mungu,*
atafunzwa naye mwongozo wa kufuata.

Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima;*
na watoto wake watamiliki nchi.

Mungu ni msiri wa watu wanaomcha;*
yeye huwajulisha hao agano lake.

Namtazamia Mungu daima anisaidie;*
yeye peke yake ataniokoa mtegoni.

Uniangalie, Ee Mungu, unionee huruma,*
kwa sababu mimi niko peke yangu, na mnyonge.

Uniondolee mahangaiko yangu;*
uniokoe katika taabu zangu.

Uangalie unyonge wangu na dhiki yangu;*
unisamehe dhambi zangu zote.

Angalia jinsi walivyo wengi adui zangu;*
ona jinsi wanavyonichukia mno.

Uyalinde maisha yangu na kuniokoa;*
nakukimbilia wewe, usikubali niaibike.

Wema na uadilifu vinihifadhi,*
maana ninakutumainia wewe.

Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;*
uwaokoe katika taabu zao zote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.

Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'

Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Mika5:4-5a
Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA, kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia. Na mtu huyu atakuwa amani yetu.

K. Mataifa yatalicha jina lako, Bwana.
W. Na wafalme wote wa dunia watatukuza utukufu wako.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Hag.2:6,9
Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema BWANA wa majeshi.

K. Utukumbuke, Ee Bwana, kwa upendo wako ulio nao kwa watu wako.
W. Njoo, utuokoe.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Mal.4:2
Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake.

K. Njoo, Ee Bwana, usikawie.
W. Uwafungue watu wako kutoka dhambi zao.

SALA:
Tuombe: Bwana, uje na utuoneshe uwezo wako. Uje, kwa uwezo wako mkuu, kutusaidia. Uwe na huruma, na utusamehe dhambi zetu, ambazo ndizo zinazochelewesha wokovu wetu, unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.