Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 26 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Heri wenye moyo safi,
Kwani watamwona Mungu;
Siri ya Bwana ni yao,
Kristo yu rohoni mwao.

Bwana aliacha mbingu,
Uzima, amani kwetu,
Anyenyekee na watu,
Mfano, Mfalme wao.

Tena anajifunua,
Kwayo roho nyenyekevu;
Nao wenye moyo safi,
Takuwa yake makao.

Heri tuitamaniyo
Ni kuwa na Wewe Bwana;.
Tupe moyo mtakatifu
Hekalu unamokaa.

ANT. I: Nitawafanya muwe mwanga wa mataifa, ili mtangaze wokovu wangu hata miisho ya dunia.

Zab.72 Kumwombea mfalme
Wakampa zawadi; dhahabu, ubani na manemane (Mt.2:11)

I
Ee Mungu, umjalie mfalme uamuzi wako,*
umpe mwana-mfalme uadilifu wako;

atawale taifa lako kwa haki,*
na maskini wako kwa adili.

Kuwe na fanaka katika nchi,*
nchi yote ijae uadilifu.

Mfalme awatetee wanyonge wa taifa,/
awasaidie watoto wa fukara,*
na kuwaangamiza watu waonevu.

Mfalme aishi muda mrefu kama jua,*
na kama mwezi, kwa vizazi vyote.

Awe kama manyunyu mashambani,*
kama mvua iinyweshayo ardhi.

Uadilifu ustawi maisha yake yote,*
na amani kwa wingi mpaka mwezi ukome.

Atawale kutoka bahari hata bahari,*
kutoka mto Eufrate hata mipaka ya dunia.

Mbele yake adui zake watamwinamia,*
nao washindani wake watalamba vumbi.

Wafalme wa Tarshishi na visiwa watamlipa kodi,*
wafalme wa Sheba na Saba watamletea zawadi.

Wafalme wote wa dunia watamheshimu,*
watu wa mataifa yote watamtumikia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nitawafanya muwe mwanga wa mataifa, ili mtangaze wokovu wangu hata miisho ya dunia.

ANT. II: Bwana atawaokoa maskini; na ataziopoa nafsi zao kutoka katika udhalimu.

II
Atamkomboa fukara anayemwomba,*
na maskini asiye na wa kumsaidia.

Atawahurumia watu dhaifu na fukara,*
atayaokoa maisha yao wenye shida.

Atawatoa katika udhalimu na ukatili,*
maana maisha yao ni ya thamani kubwa kwake.

Mfalme na aishi maisha marefu;*
apokee zawadi ya dhahabu kutoka Sheba,

watu wamwombee kwa Mungu daima,*
na kumtakia baraka mchana kutwa.

Nchi na izae nafaka kwa wingi,/
vilima vijae mavuno kama ya Lebanoni,*
na watu mijini wasitawi kama majani.

Jina la mfalme litukuke daima;*
fahari yake idumu pindi liangazapo jua.

Kwake mataifa yote yabarikiwe;*
watu wote wamwite mbarikiwa!

Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli,*
ambaye peke yake hufanya miujiza.

Jina lake tukufu litukuzwe milele;*
ulimwengu wote ujae sifa yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana atawaokoa maskini; na ataziopoa nafsi zao kutoka katika udhalimu.

ANT. III: Sasa Mungu wetu amejipatia ushindi na utawala.

WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-12a Hukumu ya Mungu
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!

Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!

Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.

Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,

watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.

Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!

Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu

akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.

Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwanakondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;

maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.

Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Sasa Mungu wetu amejipatia ushindi na utawala.

SOMO: 1Pet.1:22-23
Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, ninyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote. Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, neno la milele, ninyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele.

KIITIKIZANO
K. Bwana ni mchungaji wangu; sitapungukiwa na kitu. (W. Warudie)
K. Hunilaza katika malisho ya majani mabichi.
W. Sitapungukiwa na kitu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Bwana amewashibisha mema, wenye njaa na kiu ya haki.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana amewashibisha mema, wenye njaa na kiu ya haki.

MAOMBI
Kwa shukrani tuinue mioyo yetu kwa Mungu Baba, ambaye kwa njia ya Kristo ametujalia karama zote.
W. Bwana, uwabariki watu wako.

Ee Mungu, uwalinde Baba Mtakatifu, maaskofu wetu, na viongozi walio Wakristo:
- imarisha imani yao, mapendo yao, na ujasiri wao. (W.)

Mungu Mwenyezi, tunaiombea nchi yetu:
- ijalie iweze kukuza haki na udugu duniani. (W.)

Tunawaombea wote wanaoishi kadiri ya imani ya Kikristo:
- Baba, uwatunze hao kwa wema, na uione sura ya Mwanao mpenzi ndani Nyao. (W.)

waliojitolea kukutumikia katika maisha ya utawa:
- uwatajirishe katika ufukara wao, uwapende katika ubikira wao, na uifariji mioyo yao katika utii wao kwako. (W.)

Uwajalie pumziko la milele wale waliokufa katika Kristo:
- maana kwako kuna msamaha na utimilifu wa ukombozi. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tumwombe Baba, kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, tunapokutolea sifa jioni hii, tunakuomba kwa huruma yako, uidumishe mioyo yetu katika fikara juu ya amri zako, na utujalie mwanga na tuzo la uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.