Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 26 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT. I: Sheria ya kinywa chako ni nzuri kwangu zaidi kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

Zab.119:65-72 IX Umuhimu wa sheria ya Mungu
Umenitendea vema mimi mtumishi wako,*
kama ulivyoahidi, Ee Mungu.

Unipe hekima na maarifa,*
maana nina imani na amri zako.

Kabla ya kuniadhibu nilikosa,*
lakini sasa nashika agizo lako.

Wewe ni mwema na mfadhili;*
unifundishe kanuni zako.

Wenye kiburi wanasema uwongo juu yangu,*
lakini nashika amri zako kwa moyo wote.

Watu hao hawana akili,*
lakini mimi nafurahia sheria yako.

Nimefaidika kutokana na taabu yangu,*
maana imenifanya nijifunze amri zako.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Sheria ya kinywa chako ni nzuri kwangu zaidi kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

ANT. II: Nimemtumainia Mungu, sitaogopa; mwanadamu ananitenda nini?

Zab.56:1-6,8-13 Kumtumainia Mungu
Kristo ameoneshwa akiteseka (Mt. Jeromu)

Ee Mungu, unionee huruma,/
maana watu wananivamia.*
Wakati wote adui zangu wanizingira.

Mchana kutwa adui zangu wanishambulia;*
ni wengi mno hao wanaonipiga vita.

Ee Mungu, hofu inaponishika,*
mimi nakutumainia wewe.

Namtumainia Mungu, wala siogopi./
Ninamsifu kwa ajili ya ahadi yake.*
Binadamu watanifanya nini?

Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu;*
mawazo yao yote ni ya kunidhuru.

Wanakutana kupanga na kunivizia;/
wanachunguza yote nifanyayo;*
wananiotea kwa shabaha ya kuniua.

Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao,*
uwaangushe hao waovu kwa hasira yako.

Wewe wakujua kutangatanga kwangu;/.
umeweka kumbukumbu ya machozi yangu.*
Je, yote si yamo kitabuni mwako?

Kila mara ninapokuomba msaada wako,/
adui zangu wanarudishwa nyuma.*
Najua kwa hakika: Mungu yuko upande wangu.

Sheria uliyoweka ni muhimu zaidi kwangu*
kuliko mali zote za dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Nimemtumainia Mungu, sitaogopa; mwanadamu ananitenda nini?

ANT. III: Fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Ee Bwana.

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii yaeleza mateso ya Bwana (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;/
utukufu wako uenee duniani kote.*
Kinanda na kinubi, amkeni, nitaiamsha alfajiri.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Ee Bwana.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Gal.5:13-14
Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa mapendo. Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.“

K. Nitaishi kadiri ya amri zako, Bwana.
W. Wewe waupa moyo wangu uhuru.

SALA:
Tuombe: Bwana, wewe ambaye saa hii uliwajalia Roho Mtakatifu mitume walipokuwa wakisali, tujalie nasi neema hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Gal.5:16-17
Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka ninyi wenyewe.

K. Bwana u mwema, na njia zako zapendeza.
W. Unifundishe amri zako.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, wewe ni mwanga mtupu, na ndani mwako hamna giza. Nuru yako, kwa mng'aro wake wote, ituangaze, ili tuweze kufuata kwa furaha amri zako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Gal.5:22,23a,25
Matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.

K. Bwana, nijulishe inipasavyo kuishi.
W. Na Roho wako mwema aniongoze katika njia itakiwayo.

SALA:
Tuombe: Bwana, twakuomba utujalie tuweze kuvumilia taabu na magumu kama alivyovumilia Mwanao wa pekee, anayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.