ALHAMISI JUMA 2 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Yer.17:5-10
Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga
yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea
mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa
mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa
kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani
lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi,
Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha
matunda ya matendo yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4,6(K)40:4
1. Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SHANGILIO:
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba,
nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.
INJILI: Lk.16:19-31
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau
na kitani safi, na kula siku zote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni
pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza
ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa
na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu
aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani
mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake
majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu,
kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya;
na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi
kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu
wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao
ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema,
Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu
atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu
akifufuka katika wafu.
MAOMBI
Ee Bwana, wewe ndiwe kinga yetu na kimbilio letu. Kwa hiyo, twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie wanadamu wote unyenyekevu, ili wakukiri wewe kuwa Mwezaji wa yote na mlinzi wao.
2. Sisi sote tuthamini uhai na utu wa binadamu wenzetu kuliko mali, vyeo au sifa na mambo mengine ya kidunia
ambayo ni ya kupita tu.
3. Uwahurumie wenye shida na kuwapa mahitaji yao kwa njia ya wote wenye mapenzi mema.
4. Marehemu wetu wapokelewe kifuani pa babu yetu Ibrahimu, wapate kutawala nawe milele huko mbinguni.
Tunaomba hayo kwako wewe uliye asili ya mema yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.